Na Zitto Kabwe
 
Wiki ya Machi 18 - 22, 2014 ilianza kwa siku ya Jumanne Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji Joseph Sinde Warioba aliwaslisha rasmi Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge Maalumu la Katiba. Wiki hiyo imeishia kwa siku ya Ijumaa Rais wa Jamhuri ya Muungano ndugu Jakaya Mrisho Kikwete kutoa hotuba kwa Bunge Maalumu. Hotuba zote zimepokelewa kwa hisia tofauti kulingana na msimamo wa kila mtu kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa
kuliko zote katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya - Muundo wa Muungano. Wale wanashabikia muundo wa Serikali Tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya Jaji Warioba. Wale wanaoshabikia muundo wa Serikali mbili walifurahishwa mno na hotuba ya Rais Kikwete. Sikufurahishwa na hotuba zote mbili.
 
Nitaeleza.
 
Moja, hotuba zote mbili zilichukua muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita inayohusu muundo wa Jamhuri ya Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu suala hilo tu. Ni dhahiri suala hili ni kubwa na muhimu kwani linahusu uhai wa Dola yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo masuala kama Haki za Raia ni muhimu zaidi kwani hata uwe na muundo wa namna gani wa muungano au hata muungano wenyewe kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia kwenye katiba katiba hizo zitakataliwa tu na wananchi. Huu mtindo unaozuka wa kudhani muundo wa muungano ndio mwarobaini wa matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, umasikini, elimu ya hovyo, afya dhaifu, utatufikisha pabaya na hata kurudi tena kuandika katiba kudai haki hizo. Jaji Warioba na Rais Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi cha kwamba Katiba ni zaidi ya Muungano.
 
Pili, wote wawili Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu miundo ya Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana na misingi ama ya 'malalamiko' au 'hofu'. Jaji Warioba aliorodhesha malalamiko 11 ya upande wa Zanzibar dhidi ya Muungano na malalamiko 10 ya upande wa bara. Kimsingi malalamiko yote ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo vya upande wa Zanzibar isipokuwa lalamiko namba vii linalohusu kupotea kwa utambulisho wa Tanganyika katika muundo wa Muungano.
 
Jaji Warioba anajenga msingi wa pendekezo la Tume yake kutokana na kujibu malalamiko au maarufu kero za Muungano na anasema
"....muundo wa Serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa Serikali mbili waliotuchia waasisi siyo uliopo sasa...... waasisi walituachia Muungano wa Nchi Moja yenye Serikali mbili, na siyo Nchi Mbili zenye Serikali Mbili". Nukuu hii niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu Warioba.
 
Rais Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye hofu za kuwa na Serikali tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za kuendesha Muungano, kuzuka kwa hisia za Utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari, uwezekano wa Muungano kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi kuchukua Nchi ikipidi na kutupilia mbali katiba na Serikali ya Muungano kutokuwa na Rasilimali zake. Rais alisema 'Serikali ya Muungano ni egemezi na tegemezi' nukuu ambayo niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee wangu Jakaya Kikwete.
 
Rais Kikwete hakuniridhisha kabisa namna ya kumaliza kero za Muungano kwa muundo uliopo sasa kwani muundo huo umeshindwa kuzimaliza kwa takribani miaka 50 tangu Muungano uundwe. Haiwezekani muundo uliozalisha kero lukuki ndio utarajiwe kuzimaliza kero hizo. Kwa vyovyote vile ni lazima kuwa na muundo mpya lakini kiukweli ni lazima muundo huo mpya ujibu hofu alizoeleza ndugu Rais maana ni hofu za kweli.

Jaji Warioba hakuniridhisha na namna suala la Uraia litakavyotatuliwa kwani kutoa jibu la kubakia na 'kukubali' Nchi mbili halafu uraia mmoja kunaleta mashaka makubwa. Kama tunataka kuwa na Uraia mmoja ni lazima tuwe Nchi moja, hatuwezi kuwa na Nchi mbili uraia mmoja.
 
Vilevile vyanzo vya mapato ya Muungano ni vidogo mno kuendesha dola. Hivyo basi rasimu iliyopo mbele ya Bunge Maalumu ina mapungufu makubwa japo imetoa mapendekezo yatakayomaliza malalamiko ya Muungano.
 
Sasa kazi ya Bunge ni moja tu nayo ni kuboresha rasimu iliyopo mbeleyake ili kumaliza kero za muungano zilizopo na kujibu hoja za hofu za muundo mpya. Hakuna sababu ya kubishana kwenye takwimu za Tume, tume imefanya wajibu wake na sasa Bunge Maalumu nalo litimize wajibu wake.
 
Iwapo kama kweli tunataka kusikia Watanzania wanataka nini kwenye muundo wa Muungano, tusimamishe Bunge na twende tukawaulize kwa kura (referendum). Vingivenyo tuboreshe rasimu iliyopo na iliyotokana na maoni ya wananchi wote kwa kujibu hizo hofu muhimu alizoainisha ndugu Rais na hayo malalamiko muhimu yaliyoainishwa na Tume. Sio kazi ya Bunge Maalumu kutafuta ubora wa hotuba zilizotolewa mbele yetu bali kuona mazuri ndani ya hotuba hizo yasaidie kazi yetu Tuzingatie kuwa tusijenge Nchi kwa kujibu malalamiko na hofu tu maana hofu na malalamiko hayaishi katika dunia inayobadilika kwa kasi sana.
 
Tuamue tunataka kuwa Jamhuri ya Muungano ya namna gani. Nini sababu ya Jamhuri yetu na aina gani ya Tanzania tunataka kujenga. Tuanze kwa kutafsiri sababu ya Tanzania kuwepo na Tanzania gani tunataka kujenga kisha tutunge Katiba itakayowezesha kutufikisha huko tutakapo kufika.