Monday, March 09, 2015

RAIS KITWETE NCHINI RWANDA




Rais wa Jamhuri ya Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame amesema kuwa hatua ya Mwenyekiti wa Nchi Wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuhudhuria Mkutano wa Tisa wa Nchi Zilizoungana Kutekeleza Miradi ya Miundombinu Ukanda wa Kaskazini za Northern Corridor Projects ni hatua muhimu katika kufungua utekelezaji wa miradi ya miundomninu katika kanda nyingine za EAC.

Aidha, Rais Kagame amemshukuru Rais Kikwete kwa uamuzi wake kuhudhuria Mkutano huo uliofanyika leo, Jumamosi, Machi 7, 2015, katika Ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Serena mjini Kigali, Rwanda. Rais Kikwete amefanya ziara hiyo ya siku moja kuhudhuria Mkutano huo kwa mwaliko wa Rais Kagame.

Naye Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema kuwa ni jambo la kufurahisha kwamba Rais Kikwete ameweza kuhudhuria Mkutano wa leo, kwa sababu sasa njia imefunguka kuanza kazi ya utekelezaji wa miradi kwenye Ukanda wa Kati wa Central Corridor unaokatisha katikati ya Tanzania.

Marais Kagame na Kenyatta walikuwa wanazungumza wakati wa hotuba za ufunguzi za Mkutano huo uliofanyika kwa kiasi cha saa mbili unusu mara baada ya Rais Kikwete kuwasili Kigali akitokea Dar es Salaam kiasi cha saa sita mchana.

Akifungua Mkutano huo, Rais Kagame alisema: “Nawashukuru waheshimiwa marais wote kwa kuja. Lakini hasa hasa, namshukuru sana mwenyekiti wetu wa EAC Rais Kikwete kwa kupata muda wa kuja kujiunga nasi katika mkutano huu.”

Aliongeza Rais Kagame huku makofi yakiendelea kumkaribisha na kumshangilia Rais Kikwete: “Kuwepo kwake hapa leo, kunaongeza matumaini kuwa miradi mbali mbali na mingi zaidi katika kanda mbali mbali za nchi zetu wanachama wa EAC, sasa inaweza kutekelezwa kwa haraka zaidi. Nakushukuru sana Mheshimiwa Rais.”

Mbali na Marais Kikwete, Kagame na Kenyatta, Mkutano wa leo pia umehudhuriwa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Makamu wa Rais wa Pili wa Burundi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia.

Nchi za Kenya, Uganda,Rwanda na Sudan Kusini ndizo wanachama wa Northern Corridor na kwenye mkutano wa leo, Burundi pia imetangaza kuwa imeamua kuwa mshiriki kamili wa mikutano ya Ukanda huo badala ya kuwa msikilizaji kwa muda mrefu.

Akizungumza katika Mkutano huo, Rais Kenyatta amesema: “Tunafurahi sana kwamba Mwenyekiti wetu wa EAC yuko nasi leo kwa sababu uwepo wake utaongeza msukumo wa kutuwezesha kuanza utekelezaji wa miradi mingine hasa katika Ukanda wa Kati. Tanzania ina mengi kuchangia katika jambo hilo. Kwa mfano, umeme mwingi ambao utaanza kuzalishwa na Tanzania mwaka huu, unahitajika kwa nchi zote za EAC na Northern Corridor.”

Rais Kikwete ambaye alikuwa msikilizaji tu kwa sababu Tanzania inaendelea kuwa mwanachama wa EAC bila kuwa mshirika wa Northern Corridor amezugumza kwa ufupi tu akisema kuwa kwa sababu yeye ni mwalikwa na msikilizaji asingeweza kusema mengi.

Amewaambia viongozi wenzake: “Nakushukuru Rais Kagame kwa kunialika. Kama unavyojua, mimi ni msikilizaji tu na hivyo siwezi kusema sana. Lakini napenda kuwapongezeni nyote kwa kazi mnayoifanya. Sote tunajua kuwa hakuna utengamano bila kuendeleza miundombinu.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Kinachoendelea kule Northern Corridor kitasaidia sana katika mawazo na utekelezaji wa kazi ambayo tunajiandaa kuianza kwenye Ukanda wa Kati. Nawatakieni mafanikio zaidi na kasi ya Mwenyeji Mungu katika utekelezaji wa miradi yenu.”

Chini ya Northern Corridor nchi hizo zimebuni miradi 14, ambayo baadhi yao imeanza kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha visa moja ya kusafiria ya watalii. Nchi hizo ziliunda kundi hilo mwaka mmoja na miezi tisa iliyopita na wakuu wa nchi wanachama hukutana kila baada ya miezi miwili kwa mashauriano na maamuzi.

Rais kikwete amerejea nyumbani usiku wa leo baada ya kumalizika kwa Mkutano huo.

No comments:

Post a Comment