Monday, March 02, 2015

WAZIRI MKUU AWAJULIA HALI MAJERUHI WA AJALI MBEYA



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewatembelea askari wa Jeshi la Polisi waliolazwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mbeya kutokana na ajali waliyoipata jana wakati msafara wake ukielekea Kata ya Galula wilayani Chunya.

Waziri Mkuu aliwatembelea majeruhi hao na kuwapa pole leo asubuhi (Jumapili, Machi Mosi, 2015) kabla ya kuelekea wilayani Mbozi kuendelea na ziara yake ya Mkoa wa Mbeya. Alifuatana na mkewe Mama Tunu Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Seif Mhina.

Akizungumzia hali ya majeruhi hao, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Ismail Macha alisema jana walipokea majeruhi tisa lakini watatu walifanyiwa uchunguzi wa afya zao na kuruhusiwa na wengine sita ilibidi wawalaze na kuwafanyia uchunguzi zaidi kutokana na hali zao zilivyokuwa.

“Wengi wao walipata zaidi mshtuko ndiyo maana tukaamua kuwalaza ili tuendelee kuwapa uangalizi wa karibu… Mmoja tu ndiye amevunjika mkono wa kulia lakini wengine walipata michubuko miguuni, mikononi na usoni,” alisema.

Aliwataja waliolazwa kuwa ni Deogratius Nandi (31), Paulin Masolwa (27), Omary Hussein (24), Hamisi Haji (29) ambao wote ni wanaume. Majeruhi wa kike ni Cecilia Mussa Kabona (28) na Mwazanije Hassan (23) ambaye amevunjika mkono wa kulia. Waliopata matibabu na kuruhusiwa ni Mashaka Shabani (42), Khalifa Rashid (26) na Joel Cheja (21).

Dk. Macha alisema wanatarajia kuwaruhusu leo mchana ama kesho asubuhi kwani hali zao zinaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alisema chanzo cha ajali hiyo ni vumbi na kokoto barabarani ambazo zilifanya gari hilo la FFU lisesereke na kupinduka. Hata hivyo, alisema mwendo mdogo wa gari hilo ulisaidia kuokoa maisha ya askari hao.

“Ajali ilitokea saa 5:30 asubuhi eneo la Chang’ombe ya Mjele. Eneo lile lina kokoto kubwa kubwa ambazo zilisababisha gari lao kuserereka na kupinduka… gari halikuwa kwenye mwendo mkali ndiyo maana askari hao wamepata majeraha madogo madogo,” alisema.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Mbeya kwa kutembelea wilaya ya Mbozi ambapo mbali ya kuzungumza na wananchi, atazindua maabara Vwawa sekondari, atakagua ghala la nafaka la NFRA na kupokea taarifa ya uzalishaji na usambazaji wa miche ya kahawa kwenye kituo cha TACRI - Mbimba.



IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, MACHI MOSI, 2015

No comments:

Post a Comment