Sunday, June 21, 2015

HOTUBA FUPI YA MKURUGENZI MKUU WA SHIRIKA LA AGPAHI – BW. LAUREAN R. BWANAKUNU KWENYE UFUNGAJI RASMI WA KAMBI YA ARIEL




Ndugu,
·        Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera,
·        Mganga Mkuu (M) - Kagera,
·        Waganga Wakuu (M) – Shinyanga na Simiyu
·        Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania,
·        Meneja wa Mradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu,
·        Wafanyakazi wa AGPAHI,
·        Walezi wa Watoto,
·        Wadau mbalimbali wa Afya na Haki za Watoto, (MDH, ICAP, JHPIEGO, Red Cross, World Vision Kagera, HUYAWA (Huduma ya Watoto), Tumaini Children Centre, Uyacho Orphanage Centre, TADEPA na TACDEN)
·        Watoto wa Kambi ya Ariel,
·        Waandishi wa Habari,
·        Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.

Habarini za asubuhi !
Ndugu Mgeni rasmi, Awali ya yote napenda kutoa shukrani kwako kwa kuacha shughuli zako na kuja kujumuika na sisi hapa kwenye Kambi ya Ariel (Ariel Camp). Tunasema asante sana!

Pia napenda kuwashukuru sana walezi waliokuja na watoto toka Simiyu na Shinyanga. Vile vile napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa AGPAHI na wadau wengine kwa jitihada zao za hali na mali katika kuandaa kambi hii ya watoto. Hii ni mara ya kwanza kwa AGPAHI kuandaa kambi hii katika mkoa wa Kagera, tunafarijika sana kuwa hapa.

Ndugu Mgeni rasmi, Shirika la AGPAHI ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na watanzania na watanzania wenyewe ndio sisi hapa. Kuanzishwa kwa shirika linaloendeshwa na watanzania ilitokana na dira ya serikali ya Tanzania na ile ya wafadhili  yaani serikali ya Marekani kutaka wazawa (serikali pamoja na mashirika yasiyo ya serikali) kuendesha miradi mbalimbali inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuwa na miradi endelevu.

Shirika letu linatoa huduma katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita. Huduma zitolewazo ni pamoja na tiba na matunzo, kuzuia maambukizi ya virusi toka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma za uzazi wa mpango.  Hadi mwezi Machi mwaka huu, AGPAHI imeweza kuandikisha wateja 96,638 (wanaume 34,342 na wanawake 55,975) kwenye huduma za matunzo ambapo 6,321 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 15 na hii sawa ni asilimia 7.

Vilevile AGPAHI imeweza kuwaanzishia dawa wateja wapatao 63,048 (wanaume 21,555 na wanawake 36,969) kwenye huduma za tiba ambapo watoto ni 4,524 ambayo ni sawa na asilimia 7.

Dira ya shirika ni kuhakikisha tunatokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watoto na kuondoa UKIMWI kwa watoto. Katika kutekeleza azma hiyo shughuli mbalimbali zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoto huduma za matunzo na matibabu pamoja na huduma za kisaikolojia. Katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kuna jumla ya watoto 694,454[1] kati yao watoto 6,321 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Mgeni Rasmi, shirika la AGPAHI lilianza huduma za malezi na kuwakutanisha watoto katika vikundi vidogo vidogo baada tuu ya kuanzishwa kwake. Vikundi hivi vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya (yaani CTC) ambapo hadi sasa tuna jumla ya vikundi vipatavyo 35 (vikundi 19 kwa mkoa wa Shinyanga na vikundi 16 kwa mkoa wa Simiyu). Vikundi hivi vina jumla ya watoto 1,541.

Kutokana na kuundwa kwa vikundi hivyo, AGPAHI iliweka utaratibu wa kuendesha kambi ili kuwakutanisha watoto kutoka kwenye vikundi mbalimbali kwa lengo la kujifunza kuhusu afya na stadi za maisha na pia kubadilishana uzoefu. Kambi hizi pia huwajenga watoto na kuwafanya mabalozi wa huduma za watoto katika jamii. Kambi hizi za watoto zimekuwa zikifanyika mara moja kwa mwaka; ambapo kwa mwaka huu tumeweza kufanikisha kuwa na kambi mbili. Hii inamaanisha watoto wengi zaidi wanapata nafasi ya kushiriki kwenye kambi.

Mgeni Rasmi, kambi hii ambayo tunaifunga rasmi leo ni ya tano kufanyika na kauli mbiu ya kambi hii ni “AGPAHI inajali watoto wakue na kuishi kwenye matumaini chanya.” Kambi za awali zilifanyika katika mikoa ya Pwani, Mwanza na Kilimanjaro. Hii ni mara ya kwanza kufanyia kambi ya watoto katika Mkoa wa Kagera na tumefurahia mandhari nzuri ya mkoa huu.

Kambi hii imefanyika kwa muda wa siku tano na imekua na idadi ya watoto wapatao 57 wenye umri wa kuanzia miaka 8 hadi 17.  Watoto hawa wanatoka katika vituo mbalimbali kwenye halmashauri zote za mikoa ya Shinyanga na Simiyu.

Katika kipindi hiki cha wiki moja, watoto wameweza kujifunza mambo mbalimbali kama vile: Usafi binafsi; Stadi za maisha na Mabadiliko ya tabia kutokana na msukumo wa kundi; Taarifa sahihi kuhusu VVU na UKIMWI; Haki na wajibu watoto; Huduma na msaada wa kisaikolojia; Jinsia, mahusiano ya kimapenzi na Uzazi wa Mpango; Ufuasi mzuri wa dawa na Kuweka wazi hali yako (disclosure).
Katika wiki hii ya kambi, watoto pia wameweza kupata huduma ya kisaikolojia pamoja na kuhudumiwa na madaktari wa watoto kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania.

Mbali na mafunzo, watoto pia wamefanya matembezi na kuona mto Kagera, Kagera sugar factory, kuona na kuelezewa maeneo ya vita vya IDD AMIN na pia wamefika Mutukula (mpaka wa Tanzania na Uganda).

Ningependa kutambua washindi wa Shindano la Mr and Miss Ariel camp ambalo lilifanyika jana usiku. Washindi wetu walikua James Jackson (Mr. camp) kutoka Zahanati ya Bugarama (MSALALA) na Anastazia Daniel (Miss Camp) kutoka Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Naomba wasimame na tuwapigie makofi.

Ndugu mgeni rasmi, napenda kutoa shukrani zetu kwa Watu wa Marekani kupitia shirika lao la CDC ambao ndio wahisani wa kambi hii.   Hata hivyo tuna wafadhili wetu wengine kama EGPAF, UNFPA na USAID ambao nao wanatusaidia katika kazi zetu. Pia shirika letu linafanya kazi kwa karibu sana na ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!

LAUREAN RUGAMBWA BWANAKUNU



No comments:

Post a Comment