Tuesday, August 18, 2015

WAZIRI MKUU ATAKA SADC IWABANE WANACHAMA WAKE · Ni katika suala la uanzishaji viwanda ili kukuza uchumi




WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) haina kuweka mkakati utakaohakikisha kuwa nchi wanachama zinakuwa na mpango mahsusi wa kuendeleza viwanda kama ambavyo imekubaliwa kwenye kikao chao kilichomalizika leo.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 18, 2015), wakati akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mkutano wa 35 wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliofanyika jijini Gaborone, Botswana.

“Jumuiya ya SADC kupitia sekretarieti yake itabidi iweke mkakati maamlu wa kufuatilia kama nchi wananchama imeandaa mapango wa kuendeleza viwanda kulingana na makubaliano yaliyofikiwa kwenye kikao cha leo,” alisema Waziri Mkuu ambaye ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete.

Alisema yeye binafsi amefurahishwa na kupitishwa kwa azimio la uendelezaji wa viwanda katika nchi za SADC kwani unaendana na juhudi za Serikali ya Tanzania za kukuza uchumi kupitia uendelezaji wa viwanda vya usindikaji.

“Nimefurahi kwa sababu azimio hili linaendana na mpango wetu wa kuendeleza viwanda wa mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021. Sisi tumelenga viwanda vya kusindika mazao ya wakulima, wavuvi na wafugaji… kwa hiyo naamnini tutaenda vizuri na mpango mzima wa Jumuiya hii,” alisema.

Kuhusu madeni ya michango kutoka kwa nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, Waziri Mkuu alisema Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya ulipaji michango hiyo. “Jana nilipofika niliulizia suala hilo, nikaambiwa kwamba Tanzania imekwishalipa kwa kiwango cha kuridhisha. Nilitoa wito wakamilishe kulipa hiyo michango iliyobakia kwenye maeneo husika,” aliongeza.

Mapema, Waziri Mkuu Pinda alisoma salamu maalumu mbele ya wakuu wa nchi na washiriki wa mkutano huo zaidi ya 500, zikiwa ni salamu maalum za kuwaaga zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete. Rais Kikwete anamaliza muda wake mwishoni mwa mwaka huu na hatapata nafasi nyingine ya kushiriki kikao cha wakuu wa nchi.

Kikao kijacho kimepangwa kufanyika Agosti, 2016 nchini Lesotho ambapo Mfalme Letsie Mswati wa III alitumia fursa hiyo kuwakaribisha wakuu wa nchi wanachama kwenye mkutano huo.

Katika hatua nyingine, wakuu wa nchi  za Jumuiya ya SADC wamechangua Rais Ian Khama Seretse Khama kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo.

Katika kikao hicho waliazimia kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya Kifua Kikuu, Malaria na kuazimia kupunguza maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwenye nchi wanachama.

Mbali na kusisitiza utunzaji na uhifadhi wa mazingira, waliazimia pia kila nchi itekeleze mpango wake wa kilimo ili kuwa na akiba ya kutosha hasa ikizingatiwa hali ya ukame ambayo imezikumba nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na kuashiria uhaba mkubwa wa chakula.

Waziri Mkuu anatarajiwa kurejea nchini leo jioni.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

No comments:

Post a Comment