Monday, November 23, 2015

WAZIRI MKUU AKUTANA NA WATUMISHI WA OFISI YAKE



WAZIRI MKUU Majaliwa Kassim Majaliwa amewataka wafanyakazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu watambue  jukumu walilonalo la kuwahudumia wananchi kutokana na majukumu ya ofisi hiyo ambayo yanagusa maisha ya kila siku ya Watanzania.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa na pana sana na inahusika na shughuli za kila siku za Watanzania. Kwa hiyo tuna kazi kubwa ya kukidhi matarajio yao,” alisema.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Novemba 23, 2015) wakati akizungumza na wakuu wa taasisi, wakurugenzi na watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwenye mkutano uliofanyika ofisini kwake, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Leo ndiyo ameripoti kwa mara ya kwanza tangu alipoapishwa Ijumaa iliyopita kwenye Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Pamoja na kazi nyingine tunayo majukumu makubwa ambayo ni udhibiti, usimamizi na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali humu Serikalini. Ninataraji kupata mpango kazi kutoka kwa Mkuu wa kila idara na kila taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nitakwenda pia ofisi za TAMISEMI ili kuweka vipaumbele vyetu sawa,” alisema.

Aliwataka watumishi hao wawe tayari kutekeleza kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ambayo imekuwa ikisisitizwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili kuweza kumudu kasi ya utendaji kazi Serikali ambayo anaihimiza hivi sasa.

Alisema ana imani kuwa watumishi hao watampa ushirikiano kama ambavyo walikuwa wakiutoa kwa mtangulizi wake, Mhe. Mizengo Pinda ambaye amestaafu hivi karibuni.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,

No comments:

Post a Comment