Sunday, May 31, 2015

MAADHIMISHO YA 25 YA CHAMA CHA WANAWAKE WANASHERIA

  Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta na Balozi wa Sweden Nchini, Lennarth Hjelaker baada ya kuhutubia katika sherehe za kuadhimisha miaka 25 ya Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kwenye viwanja vya  Karimjee  jijini Dar es salaam Mei 30, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wanachama wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) baada ya kuhutubia katika sherehe za miaka 25 ya chama hicho kwenye viwanja vya  Karimjee jijini Dar es salaam Mei 30, 2015. Aliyekaa wapili kulia ni balozi wa Sweden nchini, Lennarth Hjelaker.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


MABALOZI WA TANZANIA NDANI YA MJENGO

Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi Waliotembelea Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wa kwanza kushoto ni Balozi wa Tanzania Ubeligiji, Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya Balozi Dr. Diodorus Buberwa Kamala.

Wednesday, May 27, 2015

WAZIRI MKUU JIMBONI KWAKE




Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na mtoto Albert Kanan wa darasa la tatu katika shule ya msingi ya Ilalangulu wilayani Mlele ambaye alikwenda nyumbani kwa Waziri Mkuu katika kijiji cha Kibaoni akiomba kupiga naye picha. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

The Africa Energy Forum – an important platform for project investment



456 unique companies have registered to date from 63 countries worldwide
  
With global investors clearly looking closer at the opportunities on the continent, it's exciting that already 456 unique companies have registered to date from 63 countries worldwide, spanning the value chain of Africa’s power sector - 28 of those are African countries; the largest number to date in the Forum’s 17 year history.

The Forum has 11 Ministers confirmed; among those are Ministers of Energy, Infrastructure and Finance from Benin, Ghana, Guinea, Mauritius, Mozambique, Nigeria, Senegal, Sierra Leone, Rwanda, Uganda and Zambia, as well as heads of utilities and regulators across Africa.

New for 2015:

•          This year’s Forum introduces the ‘Power In Africa Awards’ & Black Tie Gala Dinner – an ‘Emirati Banquet’ honouring people and businesses with actual projects in operation on the continent.

•          12 Ministerial and Utility-led country specific project briefings will shine the spotlight onto unique countries in Africa to provide detailed industry insights and in-country knowledge.

•          Africa Energy Yearbook- the official publication of the Forum now featuring insights from the most prolific investors and important stakeholders in the energy space.

•          Private meeting rooms for over 530 closed door meetings between investors and stakeholders.

•          Sponsored by Aggreko and Norton Rose Fulbright, the ‘EnergyNet Student Engagement Initiative (ESEI)’ brings 32 of the brightest chemical engineers and economics and law students from South Africa, Nigeria, Ghana, Mozambique, Tanzania, Kenya and Zambia to Dubai to meet investors and take that next step towards further development and employment.

•          This year also sees the launch of the ‘ESEI Innovation Hub,’ showcasing creative exciting and scalable renewable technology destined to impact Africa’s access to alternative energy solutions. 

•          Not to be missed – ‘Access Power’ present the ‘Access Co-development Fund (ACF)’; a live ‘Dragon’s Den’ style competition for early stage project investment, enabling four shortlisted projects to pitch for up to US$5m of development finance which will be awarded during the Forum in Dubai.

EnergyNet’s Simon Gosling commented; “We’re delighted to bring AEF to Dubai to enable stakeholders to capture the massive potential of Middle Eastern investment.  The response from regional investors has been unprecedented and it will be exciting to learn from them how the Emirates has successfully used its natural resources to turn its economy into a booming global empire.”

Whether you are a project looking for investment or an investor looking for project, AEF is a very strong platform to engage future partners and understand the opportunities across Africa.


WAZIRI MKUU APOKEA VITABU KUCHANGIA SHULE ALIYOSOMA



WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepokea msaada wa vitabu 895 vyenye thamani ya sh. milioni 6.5/- ikiwa ni jitihada ya wadau mbalimbali kuchangia shule ya msingi aliyosoma ya Kakuni iliyoko kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.

Waziri Mkuu amepokea msaada huo jana mchana (Jumanne, Mei 26, 2015) kwenye shule mpya ya msingi Kakuni ambayo bado inaendelea kujengwa kwenye kijiji cha Kibaoni.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu Pinda aliishukuru kampuni ya General Booksellers Ltd ya kutoka Dar es Salaam kwa msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.

“Wazo la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?”

“Nilijiuliza sana ni jambo gani ambalo naweza kulifanya la kusaidia wanakijiji wenzangu na kata nzima ya Kibaoni kama shukrani kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo. Ndipo wazo la kujenga shule niliyosoma likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu uliopita,” alisema Waziri Mkuu wakati akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi.

Mapema, akiwasilisha msaada huo, mwakilishi wa kampuni ya General Booksellers Ltd, Bw. Joachim Masaburi alisema wameamua kuchangia vitabu hivyo kwa kutambua umuhimu wa elimu kwa watoto lakini pia wanatambua juhudi za Serikali za kutoa elimu bora.

Akitoa mchanganuo wa vitabu hivyo, Bw. Masaburi alisema: “Kuna vitabu 600 kwa ajili ya shule ya awali ambavyo kati yake 300 ni vya ngazi ya chini (nursery) na vitabu vingine 300 ni vya ngazi ya juu (pre-school). Vyote ni vya hisabati, Kiingereza na sayansi”.

“Kwa shule ya msingi wao tunawapatia kivunge cha kufundishia mfumo wa mwili wa binadamu kama sehemu ya masomo ya sayansi, hiki kina thamani ya sh. 550,000/-,” alisema.

Pia kampuni hiyo ilitoa msaada wa vitabu vingine 295 vya Baiolojia, Fizikia, Uraia, Kiswahili kwa ajili ya shule ya sekondari ya Mizengo Pinda iliyoko kijijini hapo.

Hadi sasa majengo yaliyokamilika kwenye shule hiyo ni madarasa 14, jengo la utawala lenye ofisi za walimu na maktaba mbili (wanafunzi na walimu), jengo la TEHAMA la wanafunzi lenye darasa moja, ukumbi mdogo na ofisi za walimu na jengo moja la choo lenye matundu 48. Pia ujenzi wa nyumba sita za walimu uko kwenye hatua ya kuezeka. Nyumba hizo zinajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ujenzi wa choo kingine chenye matundu 48 umeanza.

Waziri Mkuu aliwaomba wananchi wengine wamsaidie kutimiza ndoto yake kwani bado anakabiliwa na kazi ya kuweka umeme, maji, kujenga nyumba nane za walimu, bwalo na jiko, karakana nne za ufundi, ujenzi wa kituo cha walimu cha mafunzo ya muda mfupi na utunzaji taarifa (Resource Centre), viwanja vya michezo vya kisasa vinavyozingatia michezo yote, mfumo wa uvunaji maji ya mvua, mfumo wa maji safi na maji taka, nyumba mbili za walinzi na uzio wa shule.

Alitaja vitu vingine ambavyo bado vinahitaji kuchangiwa ni meza za walimu – za ofisini na darasani, viti vya walimu – vya ofisini na darasani, madawati ya shule ya msingi na ya awali, meza na viti vya maktaba zote mbili, meza na viti vya bwalo – shule ya msingi na shule ya awali.



IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,

WAZIRI MKUU AJIANDIKISHA KIJIJINI KWAKE *Ahimiza kila Mtanzania ajiandikishe bila kukosa




WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka Watanzania wote watumie fursa ya uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura kwa kujiandikisha ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Akizungumza mara baada ya kujiandikisha kwenye Ofisi ya Mtendaji Kata iliyopo kijiji cha Kibaoni, wilayani Mpanda, mkoani Katavi jana jioni (Ijumaa, Mei 25, 2015), Waziri Mkuu alisema hii ndiyo fursa pekee ya kuwawezesha kushiriki uchaguzi mkuu ujao.

“Ninawasihi Watanzania wote tusiache kutumia fursa hii… kila mtu ahakikishe kuwa anajiandikisha. Ni fursa pekee itakayohakikisha kila mwananchi anashiriki uchaguzi wa kumpata Rais, Mbunge na Diwani,” alisema.

Waziri Mkuu alisema amefarijika kwa kazi aliyoiona ikifanyika kwani hadi sasa Halmashauri za Nsimbo na Mlele zimefanikiwa kuandikisha watu kwa zaidi ya asilimia 100.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya uandikishaji katika Halmashauri ya Mlele, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bw. Godwin Benne alisema walilenga kuandikisha watu 19,482 lakini hadi kufikia jana walifanikiwa kuandikisha watu 20,292 sawa na asilimia 105. Uandikishaji katika wilaya ya Mlele ulianza tarehe 18 Mei, mwaka huu.

“Mlele tuna vituo 84 katika tarafa tatu za Inyonga, Mpimbwe na Mamba. Inyonga tuna vituo 28, Mpimbwe viko 23 na Mamba viko 33.
​"​

Akifafanua zaidi, Bw. Benne alisema katika kata ya Kibaoni ambayo ina vituo sita, jana peke yake walifanikiwa kuandikisha watu 1,007 kikiwemo kituo cha Kibaoni ambacho Waziri Mkuu Pinda alijiandikisha. Alivitaja vituo vingine kuwa ni Milumba, Sungusungu, Ilalangulu, Manga na Shule ya Msingi Kakuni ambako Mama Tunu Pinda alijiandikisha jana hiyo hiyo.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, Bw. Neneka Rashid, uandikidhaji ulianza Mei 18, 2015 kwenye kata 12 na kwamba hadi kufikia jana, kata nne zilikwishaandikisha watu 12,001 sawa na asilimia 108.9 licha ya kuwa matarajio yao yalikuwa ni kuandikisha watu 11,014. Alizitaja kata hizo kuwa ni Nsimbo, Kapalala, Magamba na Uruwira.



IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Monday, May 25, 2015

Africa Day: Ideas For Africa - By Cristina Duarte, Candidate for President of the African Development Bank (AfDB)





"No other institution is better suited than the AfDB to give Africa the needed boost to reach the promised land" - Cristina Duarte*
 
ABIDJAN, Côte d’Ivoire, May 25, 2015/ -- As we celebrate Africa Day, it gives me great pleasure to congratulates our continent for the remarkable vision it has had by embarking, decades ago, in a project aimed at achieving its unity. This year's Africa Day coincides with the return to its headquarters of the prime institution of African Development -The African Development Bank (AfDB).  It is therefore timely to once more pay tribute to the founding fathers who on May 25th, 1963 established the Organization of African Unity (OAU) which was replaced, in 2002, by the current African Union.
 
 
No other institution is better suited than the AfDB to give Africa the needed boost to reach the promised land. As a candidate to lead this important organization, I am therefore pleased to call on all the stakeholders, including outside partners of the bank, to play a more coordinated and effective role in ensuring that Africa Day becomes a landmark moment not just of celebration but for sober reflexions on needed practical ideas, actions and proposals aimed at fostering Africa's Development.
 
In order to show my commitment to what can be our continent's 'Bourse d'Idees', 'Stock-Exchange for Ideas'', I am delighted to put on the table three ideas for consideration.
 
1- I call for the institution of a Prize For Women, to be named after an African Woman who made a decisive contribution to the continent's march. Such a Prize may, after consultation with relevant people, be named for instance after a respected African woman, including those who passed away, as long as they have a legacy worthy to be celebrated.
 
2-I call for the building of ecosystems within the continent that promotes innovation that could include various aspects such as innovation awards, fund for research, industrial attachments, links between academics, policy makers, entrepreneurs, and innovators...the ultimate objective for Africa is to domesticate and democratize technology as a result of a sustained effort to develop and upgrade our capacity throughout the continent focusing on Africa's indigenous capacity for Science, Technology and innovation to address our present and future problems.
 
3- I call on African institutions, working with African States, and their outside partners, to ensure that the continent's natural resources and manufactured goods carry more local value-added while reducing the imbalances in the value-chain detrimental so far to Africa.
 
I wish Africa a great present and future while vowing to being committed to making Africa's structural transformation a reality if, as I hope, I am trusted to lead our pan-african bank.
 
*Cristina Duarte is Minister of Finances and Economic Planning, and Candidate for President of the African Development Bank (AfDB). More information: http://www.cristinaduarte2015.com
 

Ufisadi:Mawaziri 4 kushtakiwa Kenya

Kutumia ujumbe kwa vyombo vya habari, mkuu wa mashtaka ya umma nchini Kenya Keriako Tobiko, hii leo amevumbua yaliyomo katika hati za kesi za mawaziri wanne.
Tume ya maadili na kupambana na ufisadi ya Kenya imependekeza waziri wa uchukuzi mMhandisi Michael Kamau na waziri wa leba Kazungu Kambi kushtakiwa na matumizi mabaya ya ofisi.
Mhandisi Michael Kamau anakumbwa na shutuma za kutumia fedha ubadhirifu wa fedha za umma na kufanya mabadiliko katika ubunifu wa barabara ambayo tiyari ilikuwa imetengenezwa na mashauri.
Kazungu Kambi naye anadaiwa keteuwa wanachama wawili katika bodi ya shirika la taifa la hazina ya uzeeni kinyume na sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari jana alasiri jumapili, afisa mkuu wa tume ya maadili na kupambana na ufisadi Halakhe Waqo, alisema kwamba mawaziri wanne waliochunguzwa ni waziri wa Uchukuzi Mhandisi Michael Kamau, waziri wa ardhi, makao na ustawi wa miji bi Charity Ngilu, waziri wa kilimo Felix Kosgei, waziri wa leba Kazungu kambi, seneta wa Nairobi Mike Sonko na mbunge .
Tume hio imemwandikia rais Uhuru Kenyatta ombi la kuongeza muda wa uchunguzi wa kesi zilizobaki.
Siku sitini ambazo walikuwa wamepewa kukamilisha uchunguzi wa ripoti hiyo zimetimia leo.

 ''Tumekuwa na shinikizo la kukamilisha kesi kwa wakati uliotolewa ila wajibu wetu wa kufanya uchunguzi wa kina ambao unaweza kustahimili uchunguzi mahakamani umetulazimu kuomba muda zaidi''alisema Halakhe Waqo
Kwa sasa tume hio imekamilisha kesi 56 kati ya 124 zilizowasilishwa kwa uchunguzi zaidi baada ya ripoti yao ya awali iliyokabidhiwa rais Kenyatta kuwasilishwa bungeni .
Kesi 21 tayari zimefikishwa kwa mkuu wa mashtaka ya umma Keriako Tobiko.
Kufikia sasa maafisa 19 wamefikishwa mahakamani na wengine 29, kulingana na afisa mkuu wa EACC, watafikishwa mahakamani siku chache zijazo katika maeneo kadhaa nchini yakiwemo Turkana, Machakos, Nyamira, Nairobi na Trans nzoia
Hata hivyo tume hii nayo pia imekumbwa na malumbano ya ndani kwa ndani ya shtuma za ufisadi, zilizosababisha kuchunguzwa kwa kiongozi wa tume hiyo na baadhi ya wanatume wake ambao hatimae walijiuzulu.
 

Basi lachomwa Burundi

Basi moja la uchukuzi limechomwa moto mjini Bujumbura Burundi na waandamanaji waliorejea mabarabarani kupinga uamuzi wa rais Pierre Nkurunziza kuwania muhula wa tatu.
Waandamanaji wanachoma moto magurudumu haswa katika eneo la Kanyosha.
Kitongoji hicho kimekuwa kitovu cha maandamano haya dhidi ya awamu ya tatu ya rais Nkurunziza.

Maandamano haya yanarejea baada ya kuuawa kwa kiongozi wa chama cha upinzani Zedi Feruzi nje ya nyumba yake katika mji mkuu Bujumbura.
Aidha wanaharakati wa upinzani nchini humo wamesitisha mazungumzo na serikali rais Pierre Nkurunziza ya kutaka kutanzua mzozo ulioko wa kisiasa.


Mzozo huo unafuatia hatua ya Nkurunziza kuwania urais kwa muhula wa tatu.
Uamuzi ambao wengi wanasema kuwa unaenda kinyume na sheria na ndio iliyosababisha kuwepo kwa jaribio la kumpindua, na maandamano ya wiki kadhaa.
Tayari zaidi ya raia 100,000 wa taifa hilo wametorokea mataifa jirani.

Thursday, May 21, 2015

BUNGENI DODOMA

 Waziri Mkuu,Mizengo Pinda akijibu maswali bugeni mjini Dodoma, Mei 21, 2015.   (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri MkuuSera Uratibu na Bunge, Jenista Mhagama akizungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, bungeni mjini Dodoma Mei 21, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuuu)
 
Waziri wa Katiba na Sheria,Dkt. Asha Rose Migiro  akiwasilisha Makadirio  ya Matumizi ya wizara hiyo , bungeni mjini Dodoma Mei 21, 2015.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 

LISHE


ZAIDI YA WANANCHI MILIONI 92 KUNDIKISHWA KWENYE DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA KATIKA MANISPAA YA BUKOBA


Monday, May 18, 2015

Nkurunziza awafuta kazi mawaziri watatu

Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewafuta kazi mawaziri watatu, huku maandamano yakiendelea katika mji mkuu kufuatia jaribio la mapinduzi, juma lililopita.

Mawaziri walioachishwa kazi ni wa Ulinzi, mashauri ya nchi za kigeni na biashara.
Mapema hii leo, polisi walifyatua risasi hewani katika mji mkuu Bujumbura, kujaribu kuutawanya umati wa vijana uliokuwa ukifanya ghasia.

WAZIRI MKUU BUNGENI DODOMA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na wabunge  kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Mei 18, 20154, Victor Mwambalaswa wa Lupa, Sylvester Mabumba  wa  Dole na Dkt. Hamisi Kigwangalla wa Nzega. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Mei 18, 2015.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Sunday, May 17, 2015

NKURUZINZA AANZA KUFUNGUKA

Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi amejitokeza kwa mara ya kwanza tangu jaribio la mapinduzi la jumatano iliyopita.
Rais Nkurunziza akihutubia waandishi wa habari katika ikulu ya Bujumbura alionya kuwa kuna tishio la shambulizi la kigaidi kutoka kwa kundi la waislamu kutoka Somalia wenye uhusiano na Al-Qaeda , Al Shabaab.
Aliwaambia wandishi wa habari wa kimataifa kuwa tishio hilo la mashambulizi sio tu kwa taifa lake bali pia kwa Kenya na Uganda .
Hata hivyo mwaandishi wa BBC aliyeko Bujumbura anasema kuwa Nkurunziza hakuzungumzia lolote kuhusu hali ilivyo nchini Burundi wala tishio la mapinduzi dhidi yake.
Aliondoka ghafla akiwa mongoni mwa msafara uliolindwa kikamilifu.
Wapinzani wake hata hivyo wanasema huenda hiyo ni njama ya rais Nkurunziza kuidhinisha makabiliano makali dhidi ya wapinzani wake ambao tayari wameagiza wafuasi wao kujitokeza kwa wingi hapo kesho kuendelea na maandamano ya kumtaka asiwanie kipindi cha tatu katika kura za urais zitakazofanyika mwezi ujao.
Al Shabab wametishia kuishambulia Burundi kufuatia mchango wake katika majDuru kutoka kwa afisi za maswala ya usalama wanje katika serikali ya Marekani na vile vile maswala ya ndani ya serikali ya Uingereza zimekariri tishio hilo la Al Shaabab dhidi ya Burundi kufuatia mchango wake katika jeshi la umoja wa Afrika Amisom huko Somalia.
Marekani tayari imeagiza raia wake kuondoka nchini humo kufuatia tishio la shambulizi la kigaidi mbali na kuzorota kwa hali ya usalama.
Wa

WAZIRI MKUU PINDA AHUDHURIA HITIMA

Mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda akifarijiwa na Mke wa makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Asha  Seif Iddi katika Sala ya Arobaini ya kifo cha Baba mzazi wa mke wa Waziri Mkuu, Marehemu Abdallah Rehani iliyofanika nyumbani kwa Marehemu, Tabata jijini Dar es salaam Mei 17, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Sheikh wa mkoa wa Dar es salaam, Alhaji Mussa Salum akizungumza katika sala ya hitima ya marehemu Abdallah Rehani, baba mzazi wa mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Tabata jijini Dar es salaam Mei 17, 2015.Kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim na kushoto ni  Mkuu wa Mkoa wa katavi, Dkt. Ibrahim Msengi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza katika sala ya hitima ya marehemu Abdallah Rehani, baba mzazi wa  mke wa Waziri Mkuu, Mama Tunu Pinda, iliyofanyika nyumbani kwa marehemu, Tabata jijini Dar es salaam Mei 17, 2015. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


RAIS WA MSUMBIJI NCHINI TANZANIA KWA ZIARA YA SIKU TATU

Rais Filipe Jacinto Nyusi akipokea shada la maua baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini 
Dar es salaam leo. Rais huyo anayefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi kama rais wa Msumbiji yuko katika ziara rasmi ya siku tatu.
Rais Filipe Jacinto Nyusi akikagua gwaride la heshima baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini 
Dar es salaam leo. Rais huyo anayefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi kama rais wa Msumbiji yuko katika ziara rasmi ya siku tatu.
Rais Kikwete akimpokea Rais Filipe Jacinto Nyusi uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini 
Dar es salaam leo. Rais huyo anayefanya ziara yake ya kwanza nje ya nchi kama rais wa Msumbiji yuko katika ziara rasmi ya siku tatu.

Thursday, May 14, 2015

DISMAS LYASSA ATANGAZA NIA YA KUWANIA UBUNGE KUPITIA CCM

Ndugu Wanahabari
Uchaguzi Mkuu wenye lengo la kuwapata Madiwani, Wabunge na Rais nchini unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu nchini.

Nimekuwa nikitembelea vijiji na kata mbalimbali za Wilaya ya Kilombero. Hivi karibuni nilitembelea kata zote za wilaya, nilizungumza na wananchi, wengi wao walinishauri kugombea Ubunge. Wananchi wanaamini kuwa kwa pamoja tutaweza kuendeleza vema gurudumu la maendeleo kwa kasi zaidi.



Wananifahamu kama mtoto wa masikini mwenzao niliyewahi kuzunguka mitaani kupiga picha ili kuendesha maisha, mtoto wa masikini niliyewahi kuwa na ofisi ya kusafisha viatu vya watu eneo la Ubungo Maziwa kwa mzee Mrisho ili niweze kupata nauli ya kwenda shule wakati huo nasoma Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE).



Maisha nayafahamu vizuri na nina uchungu nayo, natamani kushirikiana na wananchi ili kuepukana na maisha duni. Katika maisha yangu kutokula au wakati fulani kutembea kwa miguu kwenda chuo CBE na kurudi nyumbani Ubungo Maziwa (nilikuwa naishi kwa dada), lilikuwa ni jambo la kawaida, kwani maisha yalikuwa magumu mno.



Sauti ya wananchi wa Kilombero


Kilio cha wananchi pamoja na mambo mengine ni kwamba wanahitaji kiongozi kijana mwenye nguvu za kuongoza, kiongozi mwenye ujuzi wa namna ya kuongoza na kutawala, kiongozi ambaye atakuwa bega kwa bega na wananchi katika harakati za kuwaletea maendeleo wananchi. Kiongozi ambaye anajua namna ya kuongoza, siyo namna ya kuhonga au kuwalisha yamini wapiga kura, kwani wanachohitaji watu wa Kilombero ni maendeleo, siyo zaidi. Hawahitaji kiongozi ambaye ni maarufu kwa kutembelea magari ya kifahari, wanahitaji huduma za kijamii kama shule, hospitali na wao wenyewe kusaidiwa namna ya kubuni miradi ya maendeleo.



Elimu yangu ya juu ni Stashahada ya Uzamili katika Uongozi na Utawala (Postgraduate Diploma in Leadership and Governance), kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma-Dar es Salaam niliyohitimu Aprili 22, 2014. Hata hivyo nje ya elimu nimekuwa nikishughulika na masuala ya kijamii kupitia kufanya mikutano ya ana kwa ana na jamii katika masuala ya ujasiriamali, uchumba/ndoa na kadhalika.



Mojawapo sababu za wananchi kuamini kwamba ninaweza kushirikiana nao kwa ufanisi ni rekodi ambazo wananchi wenyewe wanazo juu yangu, kwani nimekuwa nao karibu katika mambo mengi ya maendeleo ikiwamo kushirikiana nao moja kwa moja au vikundi vyao hasa  vya walemavu, kina mama, vijana na kadhalika kama mshauri wao katika suala zima la namna ya kuviendesha na kuwaunganisha na taasisi au watu wa kusaidiana nao.



Kwa hivi sasa maeneo kadhaa ya Kilombero yanasaidiwa na mashirika mbalimbali yakiwamo ya nje, baadhi yake ni kutokana na jitihada zangu….nje ya uandishi wa habari, pia nimekuwa nikimiliki kampuni ya kuwaunganisha watu na vyuo vya nje ya Global Source Watch (GSW), ambayo imekuwa ikinipa fursa ya kujuana na watu wengi wa nje.

Nachukua fursa hii kutangaza rasmi kwamba nitachukua fomu ya kugombea Ubunge kutokana na kukidhi vigezo vyote ya kugombea nafasi hii kama ilivyojieleza katika Katiba ya Tanzania ibara ya 67.-(1) ambayo pamoja na mambo mengine inasema  “Bila ya kuathiri masharti yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote atakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge endapo-

(a)    ni raia wa Jamhuri ya Muungano aliyetimiza umri wa miaka ishirini na moja, na ambaye anajua kusoma na kuandika katika Kiswahili au Kiingereza;



Mimi ni mzaliwa wa Kijiji cha Mofu, wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Juni 26, 1976. Nimewahi kufanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ndani na nje ya nchi ikiwamo the Guardian Limited kama mwandishi wa kujitegemea, Uwazi kama Mhariri, Leo ni Leo kama Mhariri wa Makala, Mwananchi kama Mwandishi wa makala baadaye mhariri wa jarida la ndani ya biashara, the Media Project (Marekani) kama mchangiaji nk.



Kwa sasa ni Kiongozi wa Utafiti hapa nchini (National Lead Researcher) wa taasisi ya kimataifa iitwayo Global Integrity yenye makazi yake Marekani, pia ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanahabari, lakini maamuzi haya ya kugombea ubunge ni yangu binafsi hayana uhusiano wala hayataingiliana na sehemu yoyote ninayofanyia kazi.



Nimewahi kutembea katika nchi mbalimbali kwa lengo la kwa kusoma na kutembea, baadhi yake ni Marekani, Kenya, Uganda, Dubai, Thailand, India.



OMBI KWA WASAMARIA WEMA

Napenda kuchukua fursa hii pia kuwaomba wasamaria wema kuangalia namna ya kusaidiana na wananchi wa Kilombero kwani wakati huu njia nyingi hazipitiki kwa sababu barabara zimejaa maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha. Magari yamekuwa hayapitiki katika maeneo mengi ya Kilombero kwa sasa.



Kwa mfano sehemu kubwa ya barabara ya kutoka  Ifakara kwenda Mofu haipitiki, kiasi kwamba wagonjwa wamekuwa hawawezi kubebwa kupelekwa Ifakara ambako ndiko pekee kuna hospitali ya Wilaya, St Francis. Wapo baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakibebwa kwa kutumia baiskeli na hata pikipiki, jambo ambalo limekuwa gumu hasa kwa wajawazito.



Magari ya abiriia hasa Noah zilizokuwa zikifanya safari kutoka na kuingia Ifakara kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Kilombero yamesitisha safari kutokana na barabara kujaa maji. Yapo magari machache hasa ya mizigo ambayo nayo yanafika baadhi ya vijijini kwa shida yakiwa yamebeba mizigo na abiria hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi.



Mvua zimeathiri pia kilimo, kwani mashamba mengi yamefurika maji, huku kukiwa na njaa kwa baadhi ya wanavijiji. Hivyo nachukua fursa hii kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kusaidia wananchi wakiwamo wa vijiji vya Mofu, Ihenga, Mlimba, Chisano, Chita,  Mkula, Sanje, Uchindile na Utengule



Imetolewa leo tarehe 12, Mei 2015,

na Dismas Lyassa                                
(Mtangaza nia ya kugombea Ubunge Jimbo la Kilombero kwa tiketi ya CCM)
0754 49 8972/0712183282 








Wednesday, May 13, 2015

HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA FEDHA YA OFISI YA WAZIRI MKUU NA OFISI YA BUNGE KWA MWAKA 2015/2016



UTANGULIZI


1.            Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba kutokana na Taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Wenyeviti wa Kamati za Katiba, Sheria na Utawala; Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; Uchumi, Viwanda na Biashara na Kamati ya Masuala ya UKIMWI zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi za Serikali kwa mwaka 2014/2015 na Mwelekeo kwa Mwaka 2015/2016. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Bunge, Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mafungu ya Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambazo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Msajili wa Vyama vya Siasa kwa mwaka 2015/2016.

2.            Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, kumekuwepo na matukio mbalimbali ambayo yamewagusa Watanzania. Katika kipindi hiki Bunge lilipata msiba wa Mheshimiwa Kapteni John Damiano Komba aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, aliyefariki dunia tarehe 28 Machi, 2015. Tutamkumbuka marehemu kwa utendaji wake mzuri wa kazi na pia kwa nyimbo zake zenye mafundisho na kuvuta hisia za watu wengi pamoja na michango  yake  mizuri kwa Bunge lako Tukufu. Aidha, tarehe 20 Aprili 2015, tulipata msiba wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mheshimiwa Luteni Kanali Mstaafu, Benedict Kitenga. Vilevile, tarehe 26 Aprili 2015 tulimpoteza ndugu yetu, mpigania haki na maendeleo kwa nchi za Afrika, Brigedia  Jenerali Hashim Mbita, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji  wa  Kamati ya Ukombozi Kusini mwa Afrika. Pia, kumetokea vifo, majeruhi na uharibifu wa mali kutokana na ajali za barabarani pamoja na maafa ya mvua na mafuriko.Tunamwomba Mwenyezi Mungu awaponye haraka Majeruhi wote na aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi. Amina! Nitumie fursa hii pia kuwashukuru kwa dhati wale wote waliotoa misaada ya hali na mali kwa walioathirika na matukio hayo.

3.            Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Wajumbe wa Kamati zote za Kudumu za Bunge lako Tukufu kwa michango na ushauri waliotoa wakati wa kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali  Zinazojitegemea  na  Mamlaka  za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie fursa hii  kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala chini ya Uenyekiti  wa Mheshimiwa Jason Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini ; Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa chini ya Uenyekiti  wa Mheshimiwa  Dkt. Hamisi Andrea Kigwangala, Mbunge wa Nzega; Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara chini ya Uenyekiti  wa Mheshimiwa  Joelson Luhaga Mpina, Mbunge wa Kisesa na Kamati ya Masuala ya UKIMWI chini ya Uenyekiti  wa Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o, Mbunge wa Viti Maalum, kwa mchango wao mkubwa wakati wa uchambuzi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na  Serikali za Mitaa, Ofisi ya Bunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa. Maoni na Ushauri wao umesaidia sana kuboresha Makadirio ya Bajeti ninayowasilisha leo.

4.            Mheshimiwa Spika, mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Nne inahitimisha kipindi chake cha miaka kumi kuanzia mwaka 2005. Hivyo, katika Hotuba yangu, nitaelezea kwa muhtasari baadhi ya Mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha  takribani miaka 10 ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 na 2010. Aidha, Hotuba hii imeainisha baadhi ya kazi zilizotekelezwa na Sekta mbalimbali kwa kuzingatia MKUKUTA, Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 na Malengo ya Milenia katika kufikia Malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ya kuwa nchi ya kipato cha kati.

5.            Mheshimiwa Spika, Serikali imepata mafanikio makubwa ambayo matokeo yanaonekana katika Ukuaji Uchumi, Kuimarika kwa Huduma za Kiuchumi na Kijamii na Utawala Bora. Nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi wake mahiri katika kusimamia vizuri Serikali ya Awamu ya Nne na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 na 2010. Ninawapongeza pia Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Pia, ninampongeza Mheshimwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kusimamia vizuri utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa upande wa Zanzibar. Aidha, ninawashukuru Viongozi na Watendaji wa Wizara, Taasisi za Serikali, Mikoa, Wilaya na Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na Wananchi wote kwa kutekeleza Ilani kwa mafanikio makubwa. Ni dhahiri kwamba, mafanikio yaliyopatikana yametokana na wananchi kuikubali na kushiriki kikamilifu kuitekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
                                               

HALI YA SIASA

6.            Mheshimiwa Spika, hali ya kisiasa nchini imeendelea kuimarika, demokrasia imekua na mwamko wa Wananchi kushiriki katika shughuli za siasa umeongezeka. Idadi ya Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu imeongezeka kutoka 17 mwaka 2005/2006 hadi  22 mwaka 2014/2015. Katika mwaka 2014/2015, Chama cha Wananchi na Demokrasia (CHAWADE), Chama cha Maridhiano na Uwiano (CMU) na Chama cha Kijamaa na Uzalendo Tanzania (CKUT) vimepata usajili wa muda. Aidha, hadi kufikia mwezi Februari 2015, vyama vingine nane vimewasilisha maombi ya usajili wa muda.

7.            Mheshimiwa Spika, kukua kwa demokrasia nchini kumeambatana na changamoto mbalimbali zinazotokana na ukuaji wa Mfumo wa Demokrasia na matumizi yasiyo sahihi ya demokrasia iliyopo. Ni muhimu sote tukumbuke kwamba, demokrasia ya vyama vingi inatoa fursa kwa Viongozi na Wanachama wa Vyama vya Siasa  kujenga hoja za kunadi sera za vyama vyao ili Wananchi wafanye uamuzi sahihi. Katika kunadi Sera hizo, ni lazima kuheshimiana, kuvumiliana na kuzingatia misingi ya Sheria na Utawala Bora. Maana ya haya yote ni kupingana kwa hoja bila kupigana. Hivyo, tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu natoa wito kwa Viongozi na Wanachama wa Vyama vya Siasa na Wananchi kwa ujumla kuzingatia utii wa Katiba ya Nchi, Sheria za Nchi ikiwemo Sheria ya Vyama vya Siasa na Kanuni za Maadili ya Vyama vya Siasa ili kuhakikisha kwamba amani na utulivu uliopo nchini unaendelea kudumishwa.




ULINZI NA USALAMA


Jeshi la Wananchi wa Tanzania

8.            Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015, Serikali imeliimarisha na kuliboresha Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kulipatia zana na vifaa mbalimbali vya kijeshi pamoja na mafunzo. Jeshi limehakikisha kuwa mipaka ya nchi yetu inakuwa shwari na pia limeshiriki katika shughuli za uokozi wakati wa maafa na kuwasaidia wananchi kurejea katika hali ya awali. Pia, Serikali imekarabati miundombinu katika makambi ya jeshi na kujenga Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College). Aidha, Serikali imekamilisha ujenzi wa nyumba 3,096 kati ya nyumba 6,064 zitakazojengwa katika Awamu ya Kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000 za makazi kwa Askari katika vikosi mbalimbali nchini. Ili kuimarisha amani barani Afrika na kwingineko, Jeshi la Wananchi wa Tanzania limeshiriki katika Operesheni mbalimbali za Ulinzi wa Amani huko Darfur – Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Lebanon. Aidha, Jeshi letu limetuma Waangalizi wa Amani na Maafisa Wanadhimu katika nchi mbalimbali na kushiriki mazoezi ya pamoja katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na zile za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Ushiriki huo umewaongezea Wanajeshi wetu uwezo na uzoefu katika masuala ya ulinzi wa Kimataifa.

Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa

9.            Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2013, Serikali ilirejesha mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa Mujibu wa Sheria kwa Vijana waliohitimu Kidato cha Sita. Hadi sasa, jumla ya Vijana 31,635 wamehitimu mafunzo hayo. Kurejeshwa kwa mafunzo hayo, kumewezesha kuwajengea vijana wetu ukakamavu, uzalendo, utii na ari ya kulitumikia Taifa. Aidha, mafunzo hayo yamewajengea vijana wengi stadi na maarifa ya kujiajiri wenyewe. Hivyo, natoa wito kwa vijana waliopitia mafunzo ya JKT kutumia vizuri stadi na maarifa hayo kubuni na kuanzisha miradi mbalimbali kama njia ya kujiendeleza na kujikwamua kiuchumi.

Usalama wa Raia

10.         Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi limeendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Katika kipindi cha mwaka 2005 hadi 2015, Serikali imeliimarisha Jeshi hilo kwa kulipatia mafunzo, zana na vitendea kazi muhimu. Pia, Serikali imejenga Ofisi saba za Makamanda wa Polisi wa Mikoa na kuboresha makazi ya askari kwa kukarabati na kujenga nyumba mpya 394 na mabweni 14 katika Mikoa mbalimbali nchini. Aidha, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuhamasisha ulinzi shirikishi na usalama katika jamii kupitia Dhana ya Polisi Jamii ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao. Napenda kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi kuanzisha vikundi 8,876 vya ulinzi shirikishi nchini pamoja na Dawati la Jinsia kwenye Vituo vyote vya Polisi. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na ukarabati na ujenzi wa makazi ya askari na miundombinu  pamoja na kulipatia vifaa na vitendea kazi muhimu. Nitumie fursa hii kuwakumbusha wananchi wote kwamba msingi wa usalama wa Raia na Mali zao nchini Tanzania ni wa Watanzania wenyewe. Hivyo, tuna wajibu wa kushirikiana na vyombo vya usalama kubaini wahalifu pamoja na vitendo vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao na kutoa taarifa kwenye Vyombo vya Sheria kwani hivyo vyote vipo katika maeneo tunayoishi.

Mauaji ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi

11.         Mheshimiwa Spika, vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi na wengine kukatwa viungo kwa sababu ya imani za kishirikina vimeendelea kulitia doa Taifa letu. Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa, vitendo hivyo vilianza mwaka 2006 ambapo kulikuwa na tukio la mauaji ya mtu mmoja. Matukio hayo yaliongezeka na kufikia saba (7) mwaka 2007 na 18 mwaka 2008. Mwaka 2009 matukio hayo yalipungua kutokana na juhudi za Serikali na Wananchi za kupambana na watu wanaofanya vitendo hivyo. Mwaka huo kulikuwa na matukio tisa (9), mwaka 2010 tukio moja (1) na mwaka 2011 hapakuwa na tukio lolote. Mwaka 2012 kulikuwa na tukio moja (1); mwaka 2013 tukio moja (1), mwaka 2014 matukio manne (4) na mwaka wa 2015 tukio moja (1). Takwimu hizo zinaonesha kuwa kuanzia mwaka 2006 hadi 2015, jumla ya watu 43 wameuawa kutokana na ukatili huo. Hali hiyo imesababisha watu wenye ulemavu wa ngozi pamoja na familia zao kuishi kwa hofu, mashaka na kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Aidha, vitendo hivyo vimeleta taswira isiyo nzuri kwa nchi yetu ikizingatiwa kwamba watu wengi ndani na nje ya nchi wanafahamu kuwa Watanzania wanaishi kwa upendo, kuheshimiana na kuthamini amani, jambo ambalo nchi nyingi zinaendelea kuiga.

12.         Mheshimiwa Spika, katika kupambana na ukatili huo, jumla ya watuhumiwa 181 walikamatwa na kuhojiwa kati ya mwaka 2006 na 2015. Kati yao, watuhumiwa 133 wamefikishwa Mahakamani na kufunguliwa kesi za mauaji na 46 kwa makosa ya kujeruhi. Watuhumiwa 13 kati hao wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa, mtuhumiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kujeruhi na watuhumiwa 73 wameachiwa huru na Mahakama baada ya kukosekana kwa ushahidi. Watuhumiwa sita hawajakamatwa na upelelezi wa kesi 10 bado unaendelea. Aidha, watuhumiwa wawili waliuawa na wananchi kabla ya kufikishwa Polisi.

13.         Mheshimiwa Spika, chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani za kishirikina kwa tamaa za kupata utajiri au cheo.  Mimi siamini kwamba cheo, wadhifa, mali au utajiri hupatikana kwa njia haramu kama hizo. Utajiri hupatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa na siyo vinginevyo. Serikali itaendelea kupambana na watu wanaojihusisha na vitendo hivyo kwa nguvu zake zote. Naomba ushirikiano wa Wananchi na Viongozi wa Dini zote, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wote wa Maendeleo katika vita hivi. Aidha, niwaombe watu wote wenye mapenzi mema na nchi yetu kutoa taarifa zinazohusu vitendo hivyo kwa vyombo vya Dola ili kusaidia kubaini wahusika wote wa vitendo hivyo. Niwaombe Viongozi wa Madhehebu ya Dini kuendelea kuhubiri na kuelimisha jamii kuondokana na imani potofu za kishirikina. Ninaamini tukiunganisha nguvu zetu dhidi ya ukatili huo tutashinda.

Ajali za Barabarani

14.         Mheshimiwa Spika, ajali za barabarani zimeendelea kuongezeka nchini na kusababisha vifo, majeruhi, ulemavu wa kudumu pamoja na upotevu na uharibifu wa mali za wananchi. Hivi karibuni tumeshuhudia mfululizo wa ajali ambazo zingeweza kuzuilika. Ajali nyingi kati ya hizo zimesababishwa na uzembe wa madereva kutozingatia Sheria za Usalama Barabarani ikiwa ni pamoja na mwendo kasi, ulevi, ubovu wa magari na pia kuendesha magari bila kujali watumiaji wengine wa barabara. Kuanzia mwezi Julai, 2014 hadi Machi 2015, kulikuwa na matukio 8,072 ya ajali za barabarani ambayo yalisababisha vifo vya watu 2,883 na majeruhi 9,370. Hali hiyo siyo nzuri na haiwezi kuachwa kuendelea bila kuchukuliwa hatua madhubuti. Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Dola vinafanya utafiti wa kina kuhusu ajali hizo. Matokeo ya utafiti huo yataiwezesha Serikali kuchukua hatua stahiki. Vilevile, Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu usalama barabarani. Nawasihi madereva wote na watumiaji wengine wa barabara kuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama Barabarani ili kuiepusha nchi yetu na janga hili kubwa la ajali. Aidha, natoa wito kwa Wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa taarifa za madereva wanaokiuka Sheria za Usalama Barabarani kupitia namba za simu zilizotolewa na Jeshi hilo.

SHUGHULI ZA BUNGE, TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI, MUUNGANO, MABADILIKO YA KATIBA NA VITAMBULISHO VYA TAIFA

                                                                                         

Bunge

15.         Mheshimiwa Spika, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya Kutunga Sheria pamoja na Kuisimamia na Kuishauri Serikali. Aidha, Bunge linatekeleza Mpango Mkakati wa Muda wa Kati unaolenga kujenga uwezo wa Wabunge na Watumishi wake. Katika mwaka 2014/2015, Bunge limefanya mikutano minne ambapo Miswada ya Sheria 24 ilipokelewa na kujadiliwa. Kati ya hiyo, Miswada ya Sheria 17 ilisomwa kwa hatua zake zote na kupitishwa kuwa Sheria za Nchi, na miswada saba ilisomwa kwa mara ya kwanza. Aidha, Maazimio mawili yaliridhiwa na Kauli saba za Mawaziri ziliwasilishwa. Vilevile, maswali ya kawaida 536 ya Waheshimiwa Wabunge yaliulizwa na kujibiwa na Serikali pamoja na Maswali ya Msingi 39 ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu. Pia, Kamati za Kudumu za Bunge zimetekeleza shughuli zake kikamilifu ikiwa ni pamoja na kutembelea na kukagua Miradi ya Maendeleo.

16.         Mheshimiwa Spika, baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015 tutapata Bunge jipya la 11. Ni imani yangu kuwa  litakuwa  Bunge imara na litakaloendeleza mazuri yote yaliyofanywa na Bunge hili ambalo muda wake utamalizika katika kipindi kifupi kijacho. Ninawatakia kila la kheri wale wote wanaojipanga kugombea nafasi za ubunge katika majimbo yao ili warudi tena humu ndani baada ya Uchaguzi Mkuu. Ofisi ya Bunge itafanya maandalizi yote muhimu ya kulipokea Bunge jipya kwa kuboresha miundombinu ya Ofisi na pia kuimarisha huduma za utafiti, maktaba na sheria ili Bunge lifanye kazi zake kikamilifu.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi

17.         Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanza maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 pamoja na maandalizi ya kupiga Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa. Maandalizi hayo yanahusisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia mfumo wa Kisasa unaojulikana kama Biometric Voters Registration (BVR). Uzinduzi rasmi wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa kutumia BVR ulifanyika katika Mji wa Makambako Mkoani Njombe, tarehe 23 Februari, 2015.

18.         Mheshimiwa Spika, uboreshaji huo utahusisha kuandikisha wananchi wote wenye sifa za kuandikishwa kuwa wapiga kura. Wananchi hao ni pamoja na wale wenye vitambulisho vya mpiga kura na watu wote watakaokuwa wamefikisha umri wa miaka 18 wakati wa Uchaguzi Mkuu. Mfumo huo utaiwezesha Tume kuwa na taarifa sahihi za mpiga kura na kuondoa uwezekano wa mtu kujiandikisha zaidi ya mara moja. Utaratibu huo wa uandikishaji utaondoa malalamiko kutoka kwa wadau wa uchaguzi kuhusu udanganyifu katika upigaji kura.

19.         Mheshimiwa Spika, napenda kulikumbusha Bunge lako Tukufu na Wananchi wote kwamba, Tanzania itatumia Mfumo wa BVR kwa ajili ya uandikishaji tu na hautatumika kwa ajili ya kupiga au kuhesabu kura kama wengine wanavyoamini.  Wale wote wenye sifa watapiga kura kwa utaratibu wa kawaida wa kutumia karatasi maalum na matokeo yatatolewa na kubandikwa vituoni kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye Chaguzi zilizopita. Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea kutoa elimu, taarifa na ratiba kwa Umma kuhusu zoezi la uandikishaji linavyofanyika katika maeneo yote nchini.

20.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaendelea na zoezi la Kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kutoa elimu ya Mpiga Kura, kusimamia na kuendesha zoezi la  Kura ya Maoni kwa ajili ya Katiba Inayopendekezwa na kufanikisha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2015. Natoa wito kwa Wananchi wote wenye sifa kujiandikisha ili waweze kupiga Kura ya Maoni juu ya Katiba Inayopendekezwa na kuchagua Viongozi wao ifikapo Oktoba, 2015.
                 

Muungano

21.         Mheshimiwa Spika, Muungano wetu umedumu kwa zaidi ya nusu karne. Katika kipindi hicho tumepata mafanikio makubwa na ya kujivunia. Hii imetokana na misingi imara iliyowekwa na Waasisi wa Taifa letu pamoja na utamaduni wetu wa kujadiliana na kutatua changamoto kila zinapojitokeza. Kinachotia moyo ni kwamba, hata wakati wa mchakato wa kuandaa Katiba Mpya, mjadala ulijikita kwenye aina ya Muungano tunaoutaka na siyo kuwepo au kutokuwepo kwa Muungano. Hii inadhihirisha kuwa Muungano ni jambo muhimu na unakubalika na Watanzania wa pande zote mbili. Hivyo, tuna kila sababu ya kuulinda na kuudumisha Muungano wetu na kujivunia Utaifa tuliouanzisha sisi wenyewe.

22.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne, kupitia Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) chini ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kushughulikia hoja za Muungano. Kupitia Kamati hiyo, jumla ya hoja 15 zilipokelewa na kujadiliwa ambapo hoja tisa (9) zilipatiwa ufumbuzi na hoja sita (6) zipo katika hatua za utatuzi. Hoja zilizo kwenye hatua za utatuzi ni pamoja na Mgawanyo wa mapato ambao unajumuisha suala la mgawo wa misaada kutoka nchi za nje, misamaha ya mikopo, hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu. Hoja nyingine ni Utafutaji na Uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; Ushiriki  wa Zanzibar katika Taasisi za Nje; Ajira ya watumishi wa Zanzibar  katika Taasisi  za  Muungano;  Usajili wa vyombo vya moto na Tume ya Pamoja ya Fedha. Ni dhamira ya Serikali zetu mbili kuzipatia ufumbuzi hoja hizo haraka inavyowezekana.

23.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaanza utekelezaji wa utaratibu wa muda (interim) wa mgao wa ajira kwa Taasisi za Muungano. Aidha, itaendelea kuratibu Vikao vya Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ vya kushughulikia masuala ya Muungano; kuratibu masuala ya kiuchumi, kijamii, kisheria na mambo yanayohusiana na Katiba kwa faida ya pande mbili za Muungano. Pia, juhudi zitaendelezwa katika kutoa elimu kwa Umma na kuratibu masuala yasiyo ya Muungano kwa kuhakikisha kwamba Sekta, Wizara na Asasi zisizo za Muungano zinakutana angalau mara nne kwa mwaka.

Mabadiliko ya Katiba

24.         Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba 2011 mchakato wa kuandaa Katiba Mpya ulianza baada ya Bunge lako Tukufu kupitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Na. 8 ya Mwaka 2011. Sheria hiyo iliwezesha kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa na Wajumbe 32 kutoka pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwakilisha Makundi mbalimbali katika jamii. Tume hiyo ilifanya kazi iliyowezesha kupatikana kwa Rasimu ya Katiba Mpya na Bunge Maalum la Katiba lilijadili na kuandaa Katiba Inayopendekezwa.

25.         Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Katiba Inayopendekezwa itatakiwa kupigiwa Kura ya Maoni ili kupata ridhaa ya wananchi. Katika kufanikisha zoezi hilo, Serikali imechapisha Katiba Inayopendekezwa kwenye Gazeti la Serikali na pia imechapisha  na  kusambaza  jumla ya nakala milioni mbili za Katiba hiyo kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuisoma  na  kuielewa  vizuri. Ili wananchi wengi zaidi wapate fursa ya kuisoma Katiba hiyo, vilevile, Serikali imechapishwa kwenye magazeti ya kawaida na pia imewekwa katika tovuti mbalimbali za Serikali kwa wale ambao wanatumia mitandao. Ili kuwezesha Watanzania wenye mahitaji maalum ya kusoma, Serikali ilichapisha nakala 400  za  Katiba Inayopendekezwa  kwa  watu wa aina hiyo. Pia, nakala za Katiba Inayopendekezwa zenye maandishi makubwa zimeandaliwa kwa ajili ya watu wenye uoni hafifu. Serikali inaendelea kuelimisha umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu Katiba Inayopendekezwa na umuhimu wa kuipigia kura.

26.         Mheshimiwa Spika, upigaji wa kura ya maoni kwa Katiba Inayopendekezwa utafanyika baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukamilisha zoezi la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.  Natoa wito kwa Watanzania wote waisome Katiba Inayopendekezwa kwa makini na kuielewa vizuri ili waweze kufanya uamuzi sahihi wakati wa kuipigia kura. Nawasihi wananchi wote waliojiandikisha kutumia haki yao ya msingi na ya kikatiba kupiga kura bila kulazimishwa na mtu yeyote au kikundi chochote.

 

Vitambulisho Vya Taifa

27.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2011/2012, Serikali ilianza zoezi la usajili na utambuzi wa raia wa Tanzania na wageni waishio nchini kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).  Awamu ya Kwanza ilihusisha uandikishaji wa watumishi wa umma pamoja wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Lindi na Mtwara ambapo hadi Aprili, 2015 zaidi ya watu Milioni Tano wameandikishwa Tanzania Bara. Kwa upande wa Zanzibar, watu 600,000 wameandikishwa. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na zoezi la uandikishaji katika Mikoa iliyobaki, kujenga kituo cha kutunza kumbukumbu  pamoja na kujenga Ofisi 13 za Usajili za Wilaya Tanzania Bara na Zanzibar.

 

MASUALA YA UCHUMI    

                                                                 

Hali ya Uchumi

28.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014, uchumi ulikua kwa asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka 2006, ukuaji ambao ni mzuri ikilinganishwa na nchi nyingi zinazoendelea. Kutokana na ukuaji huo, Pato la wastani la Mtanzania limeongezeka kutoka Shilingi 360,865 mwaka 2005 hadi Shilingi 1,725,290 mwaka 2014.  Aidha, kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi katika Kaya uliofanyika mwaka 2012, umaskini wa kipato umepungua kutoka  wastani wa asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 28.2 mwaka 2012, sawa na asilimia 6.2.

29.         Mheshimiwa Spika, Mfumuko wa Bei umepungua kutoka asilimia 6.1 Machi 2014 hadi asilimia 4.3 Machi 2015. Kupungua kwa Mfumuko wa Bei kumetokana na sera nzuri za fedha, kuimarika kwa upatikanaji wa chakula, pamoja na kushuka kwa bei ya mafuta kwenye soko la dunia. Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Sekta za kipaumbele kukua kwa kushirikisha Sekta Binafsi. Sekta hizo ni pamoja na kilimo, mifugo na uvuvi.

Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano

30.         Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ya CCM ni kuifanya Tanzania kuwa Nchi yenye hadhi ya Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Ili kuhakikisha kuwa lengo hilo linafikiwa, Serikali iliandaa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Kumi na Tano (2011 - 2026) ambao unatekelezwa kwa vipindi vya Miaka Mitano Mitano. Mpango wa Kwanza wa Miaka Mitano ulianza kutekelezwa mwaka 2011/2012 na utamalizika mwaka 2015/2016. Ili kuharakisha utekelezaji wa Mpango huo, Serikali imeainisha miradi michache ya kipaumbele yenye uwezo wa kutoa matokeo makubwa kwa kipindi kifupi. Utekelezaji wa miradi hiyo unafanywa chini ya mfumo ujulikanao kama “Tekeleza  Sasa  kwa  Matokeo  Makubwa” (Big Results Now – BRN!).  Miradi  katika  maeneo  ya kipaumbele ya Elimu,  Maji, Uchukuzi, Kilimo, Nishati na Gesi Asilia, Kuongeza  Mapato  ya Serikali  imeanza  kutekelezwa  chini  ya utaratibu huo. Aidha, Serikali imeongeza eneo la Uboreshaji wa Mazingira  ya  Biashara  na  Uwekezaji katika BRN! Vilevile, uimarishaji wa upatikanaji wa huduma za afya ni eneo lingine ambalo litashughulikiwa kwa utaratibu wa BRN!

31.         Mheshimiwa Spika, lengo la Mfumo wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa ni kuhakikisha kuwa vipaumbele vya Kitaifa vyenye uwezo wa kuharakisha maendeleo vinatekelezwa kwa kasi na kuleta matokeo makubwa haraka. Katika kipindi cha mwaka mmoja wa utekelezaji wa Mfumo huo kuanzia Mwaka 2013/2014 hadi 2014/2015 mafanikio makubwa  yamepatikana.  Katika Sekta ya Elimu utekelezaji wa  miradi  na  malengo yaliyokusudiwa ulifikia asilimia 81; Maji asilimia 80, Nishati asilimia 79, Kilimo asilimia 77, Uchukuzi asilimia 64, na Utafutaji Rasilimali Fedha asilimia 54. Mawaziri wa Sekta watatoa ufafanuzi wa utekelezaji katika maeneo hayo watakapowasilisha Hotuba za Bajeti za Wizara husika katika Mkutano huu wa Bunge la Bajeti.

Maendeleo ya Sekta Binafsi

32.         Mheshimiwa Spika, Sekta Binafsi ni moja ya nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa soko. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imetekeleza Programu na Miradi mbalimbali  kwa  lengo  la  kukuza ushindani wa Sekta Binafsi nchini. Programu hizo ni pamoja na Mpango wa Kuboresha  Mazingira  ya  Biashara  na  Uwekezaji, Mradi wa Kukuza Ushindani  wa Sekta Binafsi na Mpango wa Kuimarisha  Mashauriano  na  Majadiliano  baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Programu hizo zinatekelezwa kwa  kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ili kuongeza ushiriki wa Sekta Binafsi katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa mikakati na kupata ufumbuzi wa  changamoto zinazoikabili Sekta hiyo. Dhamira ya Serikali ni kuijengea Sekta Binafsi uwezo wa kuwa mhimili wa ukuaji wa uchumi na kuongeza ushindani wake katika kuzalisha mali na kufanya biashara kwa ufanisi. Pia, Serikali imeendelea kufanya majadiliano na Sekta Binafsi kupitia Baraza la Taifa la Biashara katika ngazi za Taifa, Mikoa na Wilaya. Kwa kutumia utaratibu huo wa majadiliano, Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine hujadili masuala ya Kisera na Kisheria yanayoathiri uendeshaji wa Sekta Binafsi na kutolewa mapendekezo kwa ajili ya maboresho.
                               
33.         Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa programu hizo ni pamoja na kuanzisha Vituo vya Utoaji wa Huduma kwa Pamoja Mipakani. Kuanzishwa kwa Vituo hivyo kumewezesha huduma za kiforodha, uhamiaji, udhibiti wa ubora, viwango na usalama kupatikana katika kituo kimoja (one stop centre). Utaratibu huo ni tofauti na ule wa awali ambapo kila Taasisi ilikuwa inatoa huduma katika Kituo chake. Vilevile, kwa sasa huduma hizo hutolewa upande mmoja tu wa mpaka badala ya utaratibu  wa  awali ambapo huduma hizo zilifanyika katika pande zote mbili za mpaka. Hatua hizo zimeongeza ufanisi katika uingizaji na utoaji wa mizigo mipakani na kuongeza  kiwango   cha  biashara  baina  ya  nchi  jirani.   Hii ni pamoja na muda wa kukamilisha taratibu za kiforodha kuwa mfupi ikilinganishwa na hapo awali.

34.         Mheshimiwa Spika, ili Sekta Binafsi iweze kushamiri, ufanisi katika upatikanaji wa huduma za kifedha ni muhimu. Serikali imeimarisha usimamizi wa Sekta ya Fedha pamoja na kuongeza fursa za upatikanaji wa huduma za kifedha Mijini na Vijijini. Idadi ya Benki na Taasisi za Fedha zilizosajiliwa zimeongezeka kutoka 32 mwaka 2005 hadi 58 mwaka 2015 zikiwa na matawi 660 nchi nzima. Vilevile, upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia simu za kiganjani na Huduma za Uwakala wa Benki umekua kwa kiwango  kikubwa. Kwa mfano, kuanzia mwezi Julai, 2013 hadi Aprili 2014, jumla ya miamala Milioni 972.6 yenye thamani Shilingi Trilioni 28.3 ilifanyika kupitia mawasiliano ya simu za kiganjani. Hali hiyo imechangia kuweka mazingira wezeshi ya biashara, hususan biashara ndogo na za kati. Aidha, huduma hizo zimesogezwa karibu zaidi na Wananchi na hivyo kuongeza ufanisi. Hii ni pamoja na kutumia muda mfupi na haraka katika kupata huduma hizo na pia kuzifikisha kwa Wananchi wengi hasa Vijijini.

Uwekezaji

35.         Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada za Serikali za kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji, kati ya mwaka 2005 na 2014, Kituo cha Uwekezaji Tanzania kimesajili Miradi 7,159 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 74,274  na  kutoa  ajira  869,635.  Katika  mwaka  2014, Kituo cha Uwekezaji kilisajili miradi 698 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 11,871.6. Kati ya miradi hiyo, miradi ya wawekezaji wa ndani ilikuwa 328, miradi ya wawekezaji wa nje 211 na miradi ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje ilikuwa 159. Kati ya miradi hiyo, miradi 33 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 214.11 ilikuwa ya kilimo na ilitoa ajira 13,373. Miradi 109 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 294.72 ilikuwa ya Sekta ya Utalii na ilitoa ajira 5,436. Ili kuvutia uwekezaji zaidi katika Sekta ya Kilimo, Serikali inakamilisha Sera mahsusi itakayohusu uwekezaji katika Sekta ya Kilimo.

36.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuihamasisha Sekta Binafsi kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Miradi ya Ubia. Ili kufikia azma hiyo, mwezi Novemba 2014, Sheria ya Ubia baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ilifanyiwa marekebisho ili kurahisisha upatikanaji wa miradi husika. Kutokana na hatua hiyo, Vitengo vya Uratibu na Fedha vimeunganishwa na kuunda Kituo kimoja kwa ajili ya kuratibu utekelezaji wa miradi itakayotekelezwa kwa Ubia na Sekta Binafsi. Vilevile, Mfuko wa Kuwezesha Maandalizi ya Miradi ya Ubia umeanzishwa, na pia Sheria hiyo itaweka utaratibu mzuri wa usimamizi wa masuala ya ununuzi katika miradi ya ubia ili kuongeza ufanisi.

Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi

37.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 kwa kuwahamasisha wananchi kubaini fursa kwa ajili ya kuleta maendeleo yao na hivyo kuchangia katika ukuaji wa uchumi. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, juhudi kubwa zilielekezwa kuwajengea uwezo wajasiriamali kubuni, kuanzisha na kuendesha miradi yao ya maendeleo na kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Programu mbalimbali. Kwa mfano, kupitia Mpango wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Kuongeza Ajira ulioanzishwa mwaka 2006/2007, mikopo ya masharti nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 50.6 ilitolewa kwa Wajasiriamali 74,790. Mikopo hiyo ni endelevu kwa vile kiasi kinachorejeshwa hutolewa tena kama mikopo kwa Wajasiriamali wengine. Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Fedha na Mifuko ya Hifadhi za Jamii imewawezesha Wananchi 256,602 kupata  mikopo yenye jumla ya Shilingi Bilioni 105. Mikopo hiyo ilitolewa kupitia SACCOS, vikundi na watu binafsi na hivyo kuwanufaisha Watanzania wengi. Pia, Serikali kwa kushirikiana na Wadau imewezesha uanzishwaji wa takribani vikundi vya VICOBA 23,000 vyenye Wanachama 700,000 na mtaji wa Shilingi Bilioni 86.

38.         Mheshimiwa Spika, sambamba na hatua hizo, Serikali imetoa mafunzo ya Ujasiriamali kwa Wanachama wa SACCOS na vikundi vingine vya kijamii wapatao Milioni 1.6. Kati ya hao, Wanawake ni asilimia 53 na Wanaume ni asilimia 47. Vilevile, Serikali imeanzisha Mafunzo ya Ujasiriamali kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu ili kuwawezesha kujiajiri wenyewe kwa kutumia fursa zilizopo. Kutokana na uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa programu za uwezeshaji Wananchi kiuchumi, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wengine imeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Ufundishaji Ujasiriamali. Mwongozo huo utasaidia kutoa Mafunzo ya Ujasiriamali kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwafikia Wananchi wengi zaidi.

39.         Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba dhana ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ni pana na utekelezaji wake unahusisha Wadau wengi, Serikali imeandaa Mpango Jumuishi wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (National Multi-Sectoral Economic Empowerment Framework).  Mpango huo umeainisha majukumu ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yanayopaswa kutekelezwa na Wadau katika Sekta mbalimbali.  Serikali inaendelea kuwahimiza Wadau wote ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mamlaka za Serikali za Mitaa Nchini na Taasisi za Sekta Binafsi kujumuisha suala la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwenye Mipango na Bajeti zao za kila mwaka ili tufikie malengo yetu ya kuwafikia Wananchi wengi zaidi.

40.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuwahamasisha Wananchi kuanzisha na kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali, Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS, Benki za jamiii Vijijini (VICOBA) na vikundi vingine vya kiuchumi ili kwa umoja wao waweze kukopesheka na kuongeza nguvu zao za kiuchumi.  Vilevile, Serikali itaendeleza Program za kijasiriamali kwa Vijana nchini.

AJIRA KWA VIJANA

41.         Mheshimiwa Spika, upatikanaji wa ajira bado ni changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi nchini.  Kwa mujibu  wa  Sensa  ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, idadi ya Vijana  nchini  ni  Milioni  16.2,  sawa na asilimia 35.1  ya  Watanzania wote. Takwimu hizo zinabainisha kuwa, Vijana  walioajiriwa  katika  Sekta ya Umma ni 188,087, walioajiriwa katika Sekta Binafsi ni Milioni 1.03. Hivyo, sehemu kubwa ya vijana takribani Milioni 15 wamejiajiri katika shughuli za kilimo, mifugo, uvuvi na biashara ndogo ndogo. Hata hivyo, Vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya tija ndogo kwenye uzalishaji na biashara kutokana na matumizi ya teknolojia duni, ukosefu wa mitaji na elimu ya ujasiriamali. Ili kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imekuwa ikitoa elimu ya ujasiriamali na mikopo kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mifuko mingine ili kuwawezesha kuanzisha  au  kupanua  miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Serikali imetoa mikopo  ya  masharti  nafuu  yenye  thamani ya Shilingi Bilioni 5.8 kwa SACCOS 244 na Vikundi vya Vijana 667. Aidha,  jumla ya Vijana 20,626 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za maisha.

42.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa vijana ambao ni kundi kubwa la nguvu kazi kwa nchi yetu, Serikali itaimarisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na kutoa ajira ili fedha za mfuko huo zilenge zaidi katika kuwawezesha kiuchumi Vijana wasomi na Vijana wengineo walio tayari kujituma na kujiajiri wenyewe kwa kutumia elimu na vipaji vyao. Serikali inakamilisha mapitio ya Sera ya Taasisi Ndogo za Fedha ili kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wajasiriamali wadogo. Natoa wito kwa Vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na kutumia fursa hiyo ili waweze kupata mikopo na kuweza kujiajiri.

 

UZALISHAJI MALI


43.         Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuleta mageuzi katika Sekta ya Kilimo, yanayolenga kuongeza tija na uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula, Serikali ya Awamu ya Nne imeandaa upya Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013. Aidha, imetekeleza azma ya KILIMO KWANZA kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Kilimo; Programu ya Kuendeleza Umwagiliaji; Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya pamoja na Programu Kabambe ya Mageuzi na Modenaizesheni ya Ushirika na pia BRN! Kupitia Mipango na Programu hizo, Serikali imeongeza upatikanaji na usambazaji wa mbolea kutoka tani 241,753 mwaka 2005/2006 hadi tani 343,687 mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 42.2. Aidha, Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imeongeza upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima kutoka tani 10,477 za mwaka 2005/2006 hadi kufikia tani 32,340 mwaka 2013/2014, ikiwa ni sawa na asilimia 208.7 ya mahitaji.

44.         Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Mpango wa ruzuku ya mbolea na mbegu bora, wakulima walionufaika kwa utaratibu wa vocha wameongezeka kutoka takribani Kaya 737,000 mwaka 2008/2009 hadi Kaya Milioni 2.5 mwaka 2013/2014. Mfumo huo wa ruzuku ya pembejeo umewezesha wakulima  kuongeza  tija  katika  uzalishaji  wa  mahindi  kutoka wastani wa  gunia  5  hadi  gunia  15 kwa ekari moja; na uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa gunia 4 hadi gunia 20 kwa ekari moja.

Matumizi ya Zana Bora za Kilimo

45.         Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa zana bora za kilimo katika kuongeza eneo la uzalishaji na kumpunguzia mkulima harubu ya jembe la mkono, Serikali ilianzisha mpango wa kukopesha matrekta kwa wakulima wadogo kwa masharti nafuu. Kutokana na utekelezaji wa mipango hiyo na uhamasishaji wa Sekta Binafsi kuingiza Matrekta nchini, matrekta makubwa yameongezeka kutoka 6,168 mwaka 2005 hadi 10,064 mwaka 2014; na matrekta ya mkono (Powertillers) kutoka 166 mwaka 2005 hadi 6,348 mwaka 2014. Kuongezeka kwa zana hizo kumechangiwa na uamuzi wa Serikali wa kuingiza nchini matrekta na kuyakopesha kwa wakulima kwa bei nafuu katika Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima.

Huduma za Ugani

46.         Mheshimiwa Spika, ili kuwawezesha wakulima kupata teknolojia  za kisasa zitakazowawezesha kuongeza tija katika kilimo, Serikali imeongeza idadi ya maafisa ugani wa kilimo kutoka 3,379 mwaka 2006/2007 hadi 9,778 mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 189. Aidha, ili kuongeza mbinu shirikishi katika huduma za ugani, Mwongozo  wa  Kuanzisha na Kuendesha Mashamba Darasa kwenye Halmashauri zote nchini umeandaliwa. Mashamba Darasa yameongezeka kutoka 1,965 yenye Wakulima 51,623 mwaka 2006 hadi Mashamba Darasa 16,512 yenye jumla ya Wakulima 345,106 mwaka 2014.

47.         Mheshimiwa Spika, kutokana na juhudi za Serikali za kuongeza mbolea, mbegu bora, zana bora za kilimo na huduma za ugani, uzalishaji wa mazao nchini hususan ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005/2006 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 66.4. Ongezeko hilo, limeliwezesha Taifa kujitosheleza kwa chakula kwa wastani wa asilimia 125 mwaka 2014 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 95 mwaka 2005.

Hifadhi ya Taifa ya Chakula

48.         Mheshimiwa Spika, Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (National Food Reserve Agency - NFRA) umeongezewa uwezo wa kuhifadhi chakula kutoka tani 241,000 mwaka 2004/2005 hadi tani 246,000 mwaka 2014/2015 ili kuiwezesha Serikali kukabiliana ipasavyo na upungufu wa chakula wakati wa njaa na majanga. Kutokana na uzalishaji mkubwa wa chakula katika msimu wa 2013/2014, kuanzia mwezi Julai 2014, Serikali ililazimika kununua tani 304,514 za nafaka zikiwemo tani 295,900 za mahindi, tani 4,674 za mtama; na tani 3,940 za mpunga ili kuokoa mazao hayo yasiharibike na wakulima kupata hasara. Hadi kufikia mwezi Machi 2015, NFRA ilikuwa na tani 494,007 zilizokuwa zimehifadhiwa katika maghala yake na kiasi kingine kuhifadhiwa katika Maghala ya watu binafsi.

49.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo itabakia kuwa ya muhimu  sana  katika  nchi  yetu  kwa miaka mingi ijayo kwani  ndiyo inayotegemewa  na  Watanzania  wengi kwa ajili ya chakula na kipato. Juhudi zaidi zitawekwa katika kuikuza na kuendeleza Sekta hiyo hususan, kuwawezesha wakulima wadogo ili kilimo kiwe cha tija zaidi na kuongeza pato lao. Huu ndiyo Mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi katika miaka ya 2010 hadi 2020 ambazo zitaendelea kutekelezwa katika mwaka 2015/2016. Pamoja na  kuwawezesha  wakulima  kupata zana bora za kilimo kwa  gharama  nafuu  na kuwaunganisha na masoko, Serikali itaendelea na ujenzi wa maghala yenye uwezo wa tani 5,000 Wilaya ya Mbozi na tani 10,000 Songea Mjini. Aidha, Serikali itaanza ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos) vyenye uwezo wa kuhifadhi tani 160,000 katika maeneo mbalimbali nchini.

Mpango wa SAGCOT

50.         Mheshimiwa Spika, mwaka 2010, Serikali ilianzisha Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania – (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania - SAGCOT). Mpango huo unaohusisha ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma unalenga kuchochea uwekezaji mkubwa wa Sekta Binafsi kwa kushirikisha wakulima wadogo ili kubadili kilimo na kukifanya kuwa cha kisasa, chenye tija na cha kibiashara kwa kutumia mitaji, teknolojia na ubunifu. Ili kutekeleza azma hiyo, Kituo Maalum kinachoratibu uwekezaji wa kilimo katika eneo hilo kijulikanacho kama SAGCOT Centre kimeanzishwa. Kituo hicho kimekuwa chachu ya kuvutia uwekezaji kwenye kilimo katika ukanda huo na kuhamasisha wakulima wadogo kushiriki kikamilifu katika uwekezaji huo. Uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Mpango huo unaonesha kwamba, pale ambapo wakulima wadogo wameshirikishwa kikamilifu katika utekelezaji, tija imeongezeka kwa kiwango kikubwa kwani wakulima wadogo hupata fursa za kupata pembejeo, huduma za ugani na masoko. Kwa mfano, uwekezaji uliofanywa na Kampuni ya Kilombero Plantation Limited (KPL) katika uzalishaji wa mpunga katika shamba la Mngeta, Wilayani Kilombero umewezesha wakulima wadogo 8,000 kutoka katika Vijiji vinavyozunguka shamba hilo kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka tani mbili (2) hadi tani nane (8) kwa hekta. Wakulima hawa wadogo pia wameunganishwa na masoko na wamewezeshwa kupata pembejeo kwa uhakika zaidi.

Uendelezaji wa Miundombinu ya Masoko

51.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya masoko katika Mikoa na mipakani ili kukuza biashara ya ndani na kikanda. Ili kufanikisha azma hiyo, Serikali inatekeleza Programu ya Uendelezaji Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani Mazao na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF). Kupitia Programu hiyo, Serikali imekarabati barabara za Vijijini zenye urefu wa kilometa 555.3 kwa kiwango cha changarawe. Aidha, imejenga maghala 11 katika Halmashauri 10 yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000 za mazao kila moja. Vilevile, kupitia Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Masoko ya Mipakani, Serikali imejenga jumla ya masoko 10 katika maeneo ya kimkakati ya mipakani. Masoko yaliyojengwa ni pamoja na Nyamugali na Kagunga yaliyopo katika mpaka wa Tanzania na Burundi; na Masoko ya Mkenda na Mtambaswala yaliyopo katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji. Nitoe wito kwa wananchi kutumia fursa za masoko hayo kufanya biashara na nchi jirani ili kujiongezea kipato na kukuza mauzo yetu ya nje.

52.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaboresha miundombinu mbalimbali ya masoko kama vile barabara, maghala, huduma za fedha na kuweka huduma nyingine muhimu kama umeme, maji na ulinzi hasa katika maeneo ya masoko ya mpakani.

Maendeleo ya Sekta ya Mifugo

53.         Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuongeza tija katika Sekta ya Mifugo ili wafugaji waondokane na uchungaji na kuwawezesha kufuga kisasa. Ili kufikia lengo hilo, Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Mifugo nchini ambayo inalenga kuboresha uzalishaji wa mifugo bora, kupambana na magonjwa ya mifugo na kuimarisha miundombinu ya mifugo. Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi imekarabati na kujenga Majosho 847 na hivyo kuongeza idadi ya Majosho kutoka 2,177 mwaka 2006/2007 hadi 3,637 mwaka 2014/2015. Aidha, Serikali imetoa ruzuku ya dawa za kuogesha mifugo dhidi ya magonjwa yaenezwayo na Kupe na Mbung’o ambapo jumla ya lita milioni 1.2 za dawa zimenunuliwa. Matumizi ya dawa hizo yamechangia kupunguza vifo vya ndama kutoka wastani wa asilimia 40 mwaka 2006/2007 hadi chini ya asilimia 10 mwaka 2014/2015.

54.         Mheshimiwa Spika, kutokana na Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa Sekta Binafsi, viwanda vya kusindika maziwa vimeongezeka kutoka viwanda 22 hadi 74 kati ya mwaka 2005 na 2014. Viwanda hivyo vimeongeza uwezo wa usindikaji wa maziwa kwa siku kutoka lita 56,580 mwaka 2005 hadi lita 139,800 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia 147. Aidha, uzalishaji wa vyakula vya mifugo umeongezeka kutoka tani 559,000 mwaka 2005 hadi tani 915,000 mwaka 2013/2014; na viwanda vya kuzalisha vyakula hivyo vimeongezeka kutoka viwanda sita (6) mwaka 2005 hadi 80 mwaka 2014 vyenye uwezo wa kusindika tani milioni 1.4 kwa mwaka.

55.         Mheshimiwa Spika, nchi yetu imejaliwa kuwa na mifugo mingi ambayo ikitumika vizuri inaweza kubadili maisha ya wafugaji. Hata hivyo, tunahitaji kufanya mapinduzi makubwa katika Sekta hii ili wafugaji wetu waweze kufuga kisasa. Kazi iliyoanza ya kuzalisha mifugo bora na kuisambaza kwa wafugaji pamoja na kutenga maeneo maalum ya wafugaji itaendelezwa kwa nguvu zaidi ili kuongeza tija kwenye Sekta ya Mifugo. Vilevile, uwekezaji kwenye machinjio ya kisasa utahamasishwa ili mazao yatokanayo na mifugo yaweze kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Sekta ya Uvuvi

56.         Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya Uvuvi nchini ili kuwawezesha wavuvi kuzitumia fursa za viumbe hai vilivyomo katika bahari, maziwa na mito kuinua hali zao za maisha. Kupitia Programu hiyo, uzalishaji wa mazao ya uvuvi umeongezeka kutoka tani 341,109 mwaka 2006 hadi tani 375,158 mwaka 2014. Katika mwaka 2014/2015, tani 43,354 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo 42,100 ziliuzwa nje ya nchi na kuiingizia Serikali mapato ya Shilingi bilioni 7.5 ikilinganishwa na tani 38,574 na samaki hai wa mapambo 44,260 zilizouzwa nje ya nchi mwaka 2013/2014 na kuiingizia Serikali kiasi cha shilingi bilioni 6.1. Kutokana na sera nzuri za uwekezaji na uwezeshaji, Viwanda vya Kuchakata Samaki vimeongezeka kutoka viwanda 25 hadi 48 na maghala ya kuhifadhi mazao ya uvuvi kutoka Maghala 40 hadi 84. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016, Serikali itaimarisha ufuatiliaji na doria ili kudhibiti  uvuvi na biashara haramu katika mito, maziwa, bahari na maeneo ya mipakani.
             

Wanyamapori

57.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ndani ya Mapori ya Akiba, Hifadhi za Wanyamapori, kuimarisha ulinzi na usalama wa wanyamapori pamoja  na  kuziwezesha  jamii zinazoishi  jirani  na maeneo ya  hifadhi  kunufaika  na  rasilimali  za  wanyamapori.     Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeanzisha Mamlaka ya Wanyamapori ili kuimarisha uhifadhi na kukabiliana na ujangili nchini. Ili kuendeleza juhudi za kudhibiti  ujangili wa wanyamapori, Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo imeongeza uwezo wa Mamlaka za Serikali kwa kuwapatia vifaa vya kisasa ikiwa ni pamoja na helikopta moja, magari 35, silaha na mitumbwi minne. Vilevile, Serikali imeajiri askari wa wanyamapori 608.

58.          Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2014 Tanzania ilikuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda kuhusu kukomesha ujangili. Katika mkutano huo uliofanyika Arusha, nchi za Tanzania, Burundi, Kenya, Malawi, Msumbiji, Sudani ya Kusini, Uganda na Zambia  zilisaini Azimio la Kikanda la Kushirikiana katika Kuhifadhi na Kudhibiti Vitendo vya Ujangili. Tanzania pia ilisaini Mkataba wa Makubaliano ya Ushirikiano katika kuhifadhi ushoroba wa wanyamapori na nchi za Kenya (Serengeti-Masai Mara), Msumbiji (Selous-Niassa) na Zambia (Miombo – Mapane Woodland).

59.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kushirikiana na Wananchi kusimamia maliasili kupitia Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori na kuweka alama za wazi kwenye mipaka ya hifadhi za wanyamapori na ardhioevu. Tanzania kama Nchi, tunalo jukumu kubwa la kulinda urithi mkubwa wa wanyamapori tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu kwa nguvu zote. Jukumu hili haliwezi kuachiwa Maafisa Wanyamapori pekee, linahitaji nguvu zetu wote na viongozi kuanzia ngazi ya Vitongoji hadi Taifa. Tushirikiane kuwafichua majangili ili kuokoa Rasilimali hizo ambazo ni utajiri mkubwa kwa nchi yetu.

Ufugaji Nyuki

60.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka msukumo mkubwa katika kuendeleza ufugaji nyuki kibiashara na kuongeza tija katika kuzalisha Asali na Nta ili kuwawezesha wafugaji kujiongezea kipato. Kazi kubwa iliyofanyika ni kutoa elimu  na kuhamasisha wananchi kuanzisha vikundi na miradi ya ufugaji nyuki. Mwezi Novemba 2014, Serikali iliandaa Maonesho Maalum ya Asali ambayo yaliambatana na Kongamano la Kimataifa la Ufugaji Nyuki kwa lengo la kujadili maendeleo ya Sekta ya Ufugaji Nyuki nchini. Pia, Serikali  imeadhimisha mwaka wa tatu wa Siku Maalum ya Kitaifa ya Kutundika Mizinga iliyofanyika Wilayani Handeni, tarehe 25 Machi, 2015. Siku hii huadhimishwa Kitaifa, Kimkoa na Kiwilaya ili kuhamasisha Wananchi kuanzisha ufugaji nyuki katika maeneo yao kwa lengo la kuwapatia kipato kwa njia ambayo ni rafiki kwa mazingira.

61.         Mheshimiwa Spika, Serikali imetoa mafunzo kuhusu mbinu mpya za ufugaji nyuki, matumizi ya mizinga ya kisasa, utundikaji wa mizinga na usimamizi wa manzuki kwa Wananchi 7,320 katika Vikundi 921 vya wafugaji nyuki kutoka Vijiji 242 kwenye Wilaya 30. Vilevile, Serikali imegawa Mizinga ya kisasa 14,076 kwa Wananchi na vituo kumi (10) vya ukusunyaji asali vimeanzishwa katika Wilaya tano. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kutoa elimu ya ufugaji nyuki, kuboresha mifumo ya kukusanya maduhuli, kujenga maabara ya ufugaji nyuki na kuhimiza kuanzisha Chama Kikuu cha Ushirika cha Ufugaji Nyuki.

Utalii

62.         Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya juhudi kubwa za kutangaza vivutio vya Utalii Nchini, kuboresha huduma za kitalii hususan hoteli,  miundombinu na mawasiliano na kushiriki maonesho ya kimataifa. Vilevile, Serikali imefanikiwa kuyashawishi Mashirika ya Ndege ya Qatar Airways, Fly Dubai na Turkish Airlines kuongeza idadi ya safari zao nchini Tanzania. Juhudi hizo zimesaidia kuwashawishi watalii wengi zaidi kuitembelea Tanzania. Idadi ya watalii wa nje imeongezeka kutoka 1,095,884 mwaka 2013 hadi watalii 1,102,026 mwaka 2014/2015.  Mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 1,853 mwaka 2013 hadi Dola za Marekani 1,983 mwaka 2014, sawa na ongezeko la asilimia saba (7).

63.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Utalii ndiyo inayoongoza sasa  kuliingizia  Taifa  fedha  za  kigeni.  Hivyo, juhudi kubwa zinafanyika kuongeza kasi ya kutangaza vivutio vilivyopo  na  kuimarisha  utoaji  wa  huduma  muhimu, ikiwa ni  pamoja  na  kufundisha  watoa  huduma  mbinu  za  kisasa za kuhudumia watalii. Aidha, juhudi zaidi zinahitajika ili kufikia masoko mapya na kutangaza vivutio vingine vinavyopatikana  maeneo  ambayo  hayajatangazwa sana. Hii ni pamoja na kuhimiza utalii wa ndani kwa kuhamasisha wazawa kutembelea vivutio vingi vinavyopatikana nchini kote.

Madini

64.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Madini ni kati ya sekta muhimu zenye mchango mkubwa kiuchumi na kijamii.  Katika kipindi  cha  miaka  kumi  iliyopita,  mapato yatokanayo na madini yameongezeka kila mwaka kutokana na  mchango  wa  uchimbaji mkubwa na pia uchimbaji wa kati na mdogo. Katika kipindi hicho, thamani ya madini yaliyozalishwa  nchini  na kuuzwa nje iliongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 655.5 mwaka 2005 hadi kufikia Dola za Marekani Milioni 1,794 mwezi Desemba 2014. Ili kuwezesha Taifa kunufaika zaidi na rasilimali za madini, Serikali imekamilisha majadiliano na Wawekezaji wa Migodi mikubwa ya Geita, Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi ambapo Kampuni hizo zimeanza kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri za Wilaya husika kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa. Ulipaji wa ushuru huo umeongeza uwezo wa Halmashauri wa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo badala ya kutegemea malipo ya Dola za Marekani 200,000 kwa mwaka kama ilivyokuwa ikifanyika awali. Vilevile, majadiliano hayo yamewezesha Migodi yote mikubwa kulipa mrabaha wa asilimia 4 kama ilivyo kwenye Sheria ya Madini ya Mwaka 2010.

65.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali iliendeleza juhudi za kuboresha mfumo wa utoaji leseni za madini ikiwa ni pamoja na kujenga mfumo wa huduma za leseni kwa njia ya mtandao. Kufuatia jitihada hizo, muda wa kushughulikia maombi mapya umepunguzwa kutoka miezi 18 hadi kufikia miezi mitatu (3). Kuanzia mwezi Julai, 2014 hadi Machi 2015, jumla ya leseni 3,449 zilitolewa kwa wachimbaji wa madini ya aina mbalimbali nchini. Vilevile, Serikali  imeanzisha Ofisi mbili zaidi za Kanda ya Ziwa Nyasa (Songea) na Kanda ya Ziwa Viktoria Mashariki (Musoma)  ili  kusogeza  huduma  karibu na wananchi. Aidha, zimeanzishwa  Ofisi  nne za Afisa Madini Mkazi katika   Miji   ya   Bariadi,  Njombe,   Moshi na Nachingwea. Ni imani yangu kuwa wananchi watatumia kikamilifu huduma zinazotolewa na Maafisa wa Madini wa maeneo hayo ili waweze kunafaika na Rasilimali za madini zilizopo nchini.

Wachimbaji Wadogo wa Madini

66.         Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuwawezesha Wachimbaji Wadogo kuboresha shughuli za utafutaji, uchimbaji na kuongezea thamani madini. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa vitendo, kuwatengea maeneo maalum ya uchimbaji madini na kutoa ruzuku ya zana na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Serikali imetoa mikopo yenye masharti nafuu kwa Wachimbaji Wadogo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.4 na kutenga jumla ya kilometa za mraba 1,639 katika maeneo 22 hapa nchini kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo wa madini. Aidha, Serikali imeanzisha soko la Kimataifa la vito na usonara na imekarabati Kituo cha Jimolojia Tanzania kilichopo Jijini Arusha ili kukuza tasnia ya Uongezaji Thamani Madini Nchini badala ya madini hayo kusafirishwa nje ya nchi yakiwa ghafi. Hatua hizo zimetoa fursa kwa Wachimbaji Wadogo na wafanyabiashara wa nje kuanzisha uhusiano wa kibiashara.

Viwanda

67.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Viwanda ni mhimili muhimu katika maendeleo ya uchumi na kichocheo kikubwa cha ukuaji wa ajira. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, Sekta ya Viwanda imekua kwa wastani wa asilimia 7.7. Ukuaji huo umetokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa viwandani, hususan usindikaji wa vyakula na uzalishaji wa vinywaji, saruji, sigara na bidhaa za chuma. Katika kipindi hicho, mchango wa Viwanda Vidogo na vya Kati umeongezeka kwa kiwango kikubwa. Matokeo ya utafiti uliofanywa mwaka 2012 unaonesha kuwa, Viwanda Vidogo na vya Kati na Biashara Ndogo vinachangia asilimia 27.9 ya Pato la Taifa na vimefanikisha kuzalisha ajira za moja kwa moja kwa Watanzania zaidi ya Milioni 5.2. Hii inathibitisha kuwa Viwanda Vidogo na vya Kati vina mchango mkubwa katika Pato la Taifa. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kukuza Viwanda Vidogo na vya Kati ikiwemo kutoa msukumo zaidi kwa Viwanda vya Kuongezea Thamani ya Mazao Ghafi yanayozalishwa nchini.

68.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali imeanza kufanya Sensa ya Viwanda Nchini. Lengo la Sensa hiyo ni kupata takwimu na taarifa za kina za viwanda zitakazotumiwa kubuni na kuchukua hatua stahiki za kisera na kuandaa programu za kuendeleza Sekta ya Viwanda Nchini. Ukusanyaji wa takwimu hizo pia utatumika kuandaa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umelenga kuinua Sekta ya Viwanda nchini ili kufikiwa kwa malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025.

HUDUMA ZA KIUCHUMI


Ardhi

69.         Mheshimiwa Spika, Tanzania imekuwa na mabadiliko na mahitaji makubwa ya matumizi ya ardhi kwa watumiaji mbalimbali. Mahitaji hayo makubwa na kutokuwepo kwa Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi tangu awali vimesababisha kuongezeka kwa migogoro ya matumizi ya ardhi, ugomvi baina ya watumiaji mbalimbali na uharibifu wa mazingira. Ili kudhibiti hali hiyo, mwezi Agosti 2013, Serikali iliidhinisha Mpango wa Taifa wa Matumizi ya Ardhi (2013 – 2033). Mpango huo umeweka utaratibu mzuri na unaofaa wa Matumizi ya Ardhi kwa kuainisha Programu 12 za Matumizi ya Ardhi, Usimamizi wa Uendelezaji wa Miji na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Wilaya na Vijiji. Utekelezaji wa Programu hizo umewezesha Vijiji 1,560 vilivyopo katika Wilaya 92 kuandaliwa Mipango ya Matumizi ya Ardhi nchini.

70.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali iliahidi kuanza ujenzi wa Mfumo Unganishi wa Kuhifadhi Kumbukumbu za Ardhi (Integrated Land Management Information System - ILMIS) ambao unalenga kuboresha utaratibu wa upatikanaji wa Hatimiki za Ardhi na kusogeza huduma za upimaji, upangaji na usimamizi wa ardhi karibu na wananchi. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kazi ya ujenzi wa Mfumo huo imeanza kwa awamu. Katika Awamu ya Kwanza, Ofisi zote Nane za Kanda za Ardhi zitaunganishwa na Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi. Awamu ya Pili itahusisha kufunga Mfumo huo kwenye Ofisi za Ardhi za Halmashauri zote Nchini. Hatua hizo zitasaidia kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za ardhi, kurahisisha utoaji wa Hatimiliki na kukadiria kodi ya pango la ardhi.

71.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeendeleza juhudi za kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi, hususan baina ya wakulima na wafugaji na maeneo ya hifadhi kwa kuwezesha zoezi la kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika Vijiji vya Halmashauri kwa awamu. Halmashauri zilizohusishwa katika awamu ya kwanza ni Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero na Kiteto. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, mipaka ya Vijiji vyote imepimwa ikijumuisha Vijiji vilivyokuwa kitovu cha migogoro ya ardhi katika eneo hilo. Kazi iliyobaki ni kwa Serikali kujiridhisha na usahihi wa upimaji huo na kutoa maelekezo stahiki kabla ya zoezi hilo kuanza katika Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero. Aidha, uhakiki wa mipaka katika Wilaya za Gairo, Chemba na Bagamoyo umefanyika. Uhakiki huo ambao ulikuwa shirikishi umeondoa migogoro ya mipaka iliyokuwa inawakabili wananchi na Watendaji katika maeneo hayo. Kazi ya kuhakiki mipaka katika maeneo mengine itaendelezwa katika mwaka 2015/2016.

72.         Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba kadri idadi ya watu na shughuli za kiuchumi zinavyoongezeka, mahitaji ya ardhi nayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi, wakati ambapo eneo la ardhi linabaki lilelile. Hali hiyo imesababisha kuwepo kwa migogoro baina ya watumiaji mbalimbali wa ardhi. Kwa mantiki hiyo, sote tunatakiwa kutumia ardhi tuliyonayo kwa ufanisi na tija zaidi. Serikali itaendeleza juhudi za kupima ardhi na kuweka mipango bora  ya matumizi yake sambamba na kutoa elimu ya kutumia ardhi ndogo kuzalisha kisasa zaidi. Ni muhimu watumiaji wote wa ardhi wakashirikiana na Serikali kuweka mipango endelevu itakayohakikisha kwamba kila mmoja ananufaika na ardhi iliyopo kwa maendeleo na ustawi wa jamii na Taifa kwa ujumla.

 

Barabara, Madaraja na Vivuko

73.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya imefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuboresha mtandao wa barabara na madaraja nchini.  Tangu ilipoingia madarakani mwaka 2005, Serikali ya Awamu ya Nne imekamilisha ujenzi wa barabara zenye urefu wa Kilometa 1,226 zilizoanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tatu. Aidha, jumla ya Kilometa 1,305 za barabara kuu zimejengwa upya kwa kiwango cha lami na Kilometa 960 kufanyiwa ukarabati. Vilevile, Kilometa 393 za Barabara za Mikoa zimejengwa kwa kiwango cha lami. Hivyo, jumla ya barabara kuu na za mikoa zilizojengwa na kukarabatiwa kwa kiwango cha lami katika kipindi hicho ni Kilometa 3,884 na Kilometa 6,636 zimekarabatiwa kwa kiwango cha changarawe.

74.         Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa barabara mpya, Serikali pia imeendelea  kujenga madaraja madogo na makubwa katika maeneo mbalimbali nchini. Kati  ya  mwaka  2006  na  2015, Serikali imekamilisha ujenzi wa madaraja makubwa ikiwa ni pamoja na la Mwatisi (Morogoro), Ruvu (Pwani), Nangoo (Mtwara), Nanganga (Mtwara), Ruhekei (Ruvuma) na Daraja la Kikwete katika Mto Malagarasi (Kigoma). Aidha, ujenzi wa madaraja mengine makubwa sita ya Kigamboni, Mbutu, Maligisu, Kavuu, Kilombero na Sibiti unaendelea.

75.         Mheshimiwa Spika, Serikali  imekarabati na kununua Vivuko vipya kwa ajili ya kurahisisha usafiri wa majini nchini. Vivuko vilivyofanyiwa ukarabati ni pamoja na  MV Ukara, MV Sabasaba, MV Kome na MV Geita vyote vya Mwanza na MV Chato (Geita). Vivuko vipya vilivyonunuliwa ni pamoja na  MV Ruvuvu (Kagera), MV Ujenzi (Mwanza),  MV Musoma (Mara), MV Kilambo (Mtwara)  na MV Malagarasi (Kigoma).  Pia, Serikali imenunua Vivuko kwa ajili ya Kahunda – Maisome (Mwanza), Msangamkuu (Mtwara) na Kivuko cha  Dar es Salaam - Bagamoyo kitakachosaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

76.         Mheshimiwa Spika, kazi iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne kwenye ujenzi wa barabara, madaraja na vivuko ni kubwa na ya kujivunia. Nchi yetu sasa imeunganishwa na mtandao wa barabara za lami kutoka kona moja ya nchi hadi nyingine. Muda wa kusafiri na kusafirisha mizigo nchini na nchi jirani umepungua sana. Kazi hii inahitaji kuendelezwa kwa nguvu na kasi zaidi kwa miaka ijayo ili hatimaye mikoa na wilaya zote ziunganishwe kwa barabara za lami. Hivyo, kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 3,419 ambazo zipo kwenye hatua za usanifu itaendelea kufanywa na Serikali ili barabara hizo zikamilishwe.

Reli

77.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeboresha miundombinu ya Reli ya Kati kwa kununua vifaa mbalimbali zikiwemo injini mpya (locomotives) 13 za treni, Mabehewa mapya 22 ya abiria, Mabehewa 150 ya mizigo, Mabehewa 34 ya breki, Mabehewa 25 ya kubebea kokoto na Mtambo wa kunyanyulia mabehewa. Aidha, imekarabati injini saba (7) za treni, mabehewa 82 ya mizigo na mabehewa 31 ya abiria pamoja na kukamilisha kazi ya kujenga upya injini nane (8) za treni katika Karakana ya Reli iliyopo Morogoro. Kazi ya upembuzi wa kina wa ujenzi wa reli mpya ya Dar es Salaam – Isaka – Kigali/Musongati kwa kiwango cha standard gauge ilikamilika Aprili, 2014. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na mpango wa kuimarisha na kuboresha vitendea kazi na huduma katika Reli ya Kati. Aidha, itaanzisha huduma ya block train ya kusafirisha mizigo ya nchi za Rwanda, Burundi na Uganda.

Bandari

78.         Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina fursa kubwa ya kuongeza mapato kutokana na huduma za Bandari ikizingatiwa kuwa tunazungukwa na nchi sita ambazo hazina bandari. Kwa kutambua fursa hiyo, Serikali imeimarisha bandari zake ili ziweze kutoa huduma kwa ufanisi na tija. Kupitia Mpango wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa, Serikali inatekeleza miradi muhimu ambayo imesaidia kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia mizigo kutoka tani milioni 12 mwaka 2012 hadi tani milioni 14.6 mwaka 2014/2015. Vilevile, muda wa meli kukaa bandarini umepungua kutoka wastani wa siku 6.3 mwaka 2012 hadi wastani wa siku 2.9 Januari, 2015. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaanza ujenzi wa bandari mpya ya Mbegani Bagamoyo itakayokuwa kubwa kuliko bandari zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Aidha, Serikali itaendelea kuimarisha bandari za Tanga na Mtwara na zile za maziwa ili ziweze kutoa huduma bora kwa ufanisi zaidi.

Viwanja vya Ndege

79.         Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya jitihada kubwa kuimarisha usafiri wa anga kwa kujenga, kupanua na kukarabati viwanja vya ndege na kuweka mazingira mazuri kwa  Sekta  Binafsi kutoa huduma za usafiri wa anga.  Viwanja vya ndege vya Arusha, Bukoba, Kigoma, Mafia, Mpanda, Musoma, Mwanza na  Tabora vimekarabatiwa. Aidha, Kiwanja kipya cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe, Mbeya kimejengwa na kuanza kutoa huduma mwezi Januari 2013. Kazi ya kupanua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwa kujenga jengo la tatu la abiria (Terminal III) imeanza na Awamu ya Kwanza inayohusisha ujenzi wa jengo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni 3.5 kwa mwaka inatarajiwa kukamilika Oktoba, 2015.

80.         Mheshimiwa Spika, kuimarika kwa Viwanja vya Ndege nchini kumewezesha kampuni zinazotoa huduma za usafiri wa anga ndani na nje ya nchi kuongezeka kutoka 29 mwaka 2005 hadi 55 hivi sasa. Ongezeko hilo limeendana na ongezeko la abiria wanaowasili na kuondoka katika Viwanja vya Ndege nchini kutoka Abiria  milioni 2.2 mwaka 2005 hadi zaidi ya Abiria milioni 4.7 hivi sasa. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kutekeleza mradi wa  ujenzi wa jengo la tatu la abiria la Kiwanja cha Ndege cha  Julius Nyerere pamoja na kuendelea na ukarabati wa Viwanja vingine vya ndege nchini.

Nishati

81.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi ya kuimarisha upatikanaji wa umeme kupitia Mpango wa Changamoto za Milenia katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe na Tanga. Serikali pia, imekamilisha kwa asilimia 84 utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Kufua Umeme wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 150 kwa kutumia gesi asilia. Utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mradi wa Kinyerezi utakaozalisha Megawati 300 unaendelea. Vilevile, Serikali imesaini Mkataba wa utekelezaji wa Mradi wa Kufua Umeme kutoka Mto Rusumo utakaozalisha Megawati 80 kwa lengo la kuyapatia umeme wa uhakika maeneo yaliyo nje ya Gridi ya Taifa,  hususan Mikoa ya Kagera na Kigoma.

82.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha miundombinu ya uzalishaji umeme nchini kwa kiwango kikubwa na kuwezesha uzalishaji wa umeme kuongezeka kutoka Megawati (MW) 891 mwaka 2005 hadi MW 1,226.3 Machi, 2015. Ili kuongeza kasi ya kusambaza umeme Vijijini, Serikali ilianzisha Wakala wa Nishati Vijijini (Rural Energy Agency - REA) Oktoba 2007. Wakala umetekeleza miradi mingi kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini. Katika Awamu ya Kwanza ya utekelezaji wa mradi huo, Wilaya 17 zimeunganishiwa huduma za umeme na kufanya  Makao Makuu ya Wilaya zilizopata umeme kufikia 120 kati ya Wilaya 133 zilizopo. Aidha, kupitia REA, Serikali imepeleka umeme kwenye maeneo mbalimbali ya uzalishaji mali na huduma za jamii na Vijiji 3,734. Vilevile, jumla ya Shule za Sekondari 1,845; zahanati na Vituo vya Afya 898 na Hospitali 96 zilipatiwa umeme katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara. Awamu ya pili inaendelea kutekelezwa kwa lengo la kufikisha umeme katika makao makuu ya Wilaya zote nchini na maeneo mengi ya Vijijini na Mijini.

83.         Mheshimiwa Spika, sambamba na juhudi hizo, Serikali ilichukua hatua nyingine ya kupunguza gharama za kuunganisha umeme Mijini na Vijijini kwa kiwango kikubwa kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya wananchi. Kwa upande  wa  wateja  waishio Vijijini  walio  nje  ya  Mpango wa REA, gharama zilipunguzwa kutoka Shilingi 455,108/= hadi Shilingi 177,000/= na kwa maeneo ya Mijini, gharama zilipungua kutoka Shilingi 455,108/= hadi Shilingi 320,960/= kwa wateja wanaojengewa njia moja (single phase) kwa umbali usiozidi Meta 30 bila kuhitaji nguzo. Kwa miradi  inayotekelezwa na Wakala wa Usambazaji Umeme Vijijini, gharama  za uunganishwaji umeme zilipunguzwa hadi kufikia Shilingi 27,000/= tu kwa kipindi ambacho Mkandarasi anakuwa  kwenye  eneo  la  mradi. Jitihada hizo zimechangia kuongeza idadi ya Wananchi wanaopata huduma za umeme nchini kutoka asilimia 13 ya Watanzania wote mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 36 mwezi Machi, 2015 na hivyo kuvuka lengo la Ilani ya Uchaguzi ya CCM la kufikia asilimia 30 mwaka 2015.

Gesi Asilia

84.         Mheshimiwa Spika, ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia nchini umeiweka Tanzania katika orodha ya nchi zinazozalisha Gesi Asilia nyingi duniani na kutoa matumaini makubwa ya kukuza uchumi wetu. Hadi kufika Desemba, 2014, Gesi Asilia yenye Futi za Ujazo Trilioni 53.28 ilikuwa imegunduliwa na kazi ya utafutaji inaendelea. Kiasi hiki ni takriban mara tano ya Gesi Asilia iliyokuwa imegunduliwa mwaka 2005. Kutokana na ugunduzi huo, Serikali imetunga Sera ya Gesi Asilia ya Mwaka 2013 na kuandaa Muswada wa Sheria ya Gesi Asilia ili kuhakikisha kunakuwepo usimamizi imara wa Sekta ya Gesi Asilia nchini, na kuwawezesha wananchi kunufaika kikamilifu na rasilimali za Gesi Asilia.

85.         Mheshimiwa Spika, ili Taifa liweze kunufaika na rasilimali hiyo,  Serikali inatekeleza Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia lenye urefu wa Kilometa 542   kutoka   Mtwara   na  Lindi  hadi  Dar es Salaam  kupitia  Somanga   Fungu.  Utekelezaji wa mradi huo ulioanza mwezi Julai,  2012  ulikuwa  umefikia  asilimia  98 mwezi   Machi,   2015   na   utakamilika  mwezi  Julai,  2015. Vilevile, ujenzi wa mitambo ya kusafisha gesi asilia katika maeneo ya Madimba Wilayani Mtwara Vijijini na Songo Songo Wilayani Kilwa unaendelea. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaongeza uwezo wa kufua umeme hasa unaotokana na Gesi Asilia na nishati jadidifu. Vilevile, itaongeza kasi ya kupeleka umeme Vijijini pamoja na kupunguza kiwango cha upotevu wa umeme katika Gridi ya Taifa. Lengo ni kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata umeme wa uhakika.

Huduma za Mawasiliano

86.         Mheshimiwa Spika, Sekta ya Mawasiliano inakua kwa kasi na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu. Idadi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu nchini imeongezeka  kutoka laini za simu za kiganjani milioni 2.9 mwaka 2005 hadi kufikia milioni 32 mwezi Desemba, 2014. Gharama za kupiga simu zimepungua katika kipindi hicho kutoka Shilingi 112 hadi Shilingi 34.9 kwa dakika. Kupungua kwa gharama hizo kumetokana na Sera na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowezesha kuongezeka kwa watoa huduma na hivyo kuongeza ushindani wa kibiashara. Pamoja na mazingira hayo mazuri, uamuzi wa Serikali kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umewezesha watoa huduma kutumia huduma za mkongo huo badala ya kila mmoja kujenga miundombinu yake. Aidha, kumekuwa na ongezeko la huduma nyingine kupitia mawasiliano ya simu za mkononi kama vile, miamala ya kifedha na ununuzi wa huduma na bidhaa kwa kutumia miamala ya kibenki. Inakadiriwa kuwa watumiaji wapatao milioni 12.3 wanatumia huduma za miamala ya kibenki kwa kutumia simu za kiganjani. Vilevile, watumiaji wa huduma za intaneti wameongezeka kutoka milioni 3.6 mwaka 2008 hadi watumiaji milioni 11.3 mwaka 2014.

87.         Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha  Awamu ya Kwanza na ya Pili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 7,560 ambao uliunganisha Makao Makuu ya Mikoa yote Tanzania, baadhi ya Makao Makuu ya Wilaya na pia kuunganisha na nchi jirani.  Awamu ya Tatu ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa utaziunganisha Wilaya zote nchini na kukamilisha uunganishaji wa maeneo ya Unguja na Pemba. Awamu hiyo itahusisha pia ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu katika Jiji la Dar es Salaam, Zanzibar na Dodoma. Katika Awamu ya Nne, Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano ambao ni Airtel, Tigo, Vodacom  na  Zantel, inajenga Mikongo ya Mijini (Metro Fibre Ring Networks), ambapo hadi mwezi Machi 2015, jumla  kilomita 91 zilikuwa zimekamilika katika Jiji la Dar es Salaam. Aidha, ujenzi wa Mikongo unaendelea katika Miji ya Arusha na Mwanza ambapo jumla ya kilomita 94 zimejengwa. Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano utakapokamilika, utawezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa haraka zaidi, uhakika na kwa gharama nafuu. Vilevile, utaboresha mawasiliano baina ya Tanzania na nchi jirani pamoja na nchi nyingine duniani baada ya kuunganishwa na Mikongo ya Kimataifa ya SEACOM, EASSy na SEAS ambayo tayari imefika hapa nchini.

88.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeingia Makubaliano ya Ushirikiano na Kampuni ya VIETTEL (Viettel Joint Stock Company – VIETTEL) ya Vietnam kuwekeza katika maeneo yasiyokuwa na mawasiliano vijijini. Kampuni hiyo itajenga kwa awamu miundombinu ya Mkongo wenye urefu wa kilometa 13,000 kwa kutumia teknolojia rahisi katika Wilaya zote  nchini pamoja na kujenga miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa na mawasiliano. Vilevile, Kampuni hiyo itaziunganisha Ofisi za Wakuu wa Wilaya, Hospitali za Wilaya, Ofisi za Polisi za Wilaya na Ofisi 65 za Posta  katika  mkongo pamoja na  kupeleka na kutoa huduma  za  intaneti  bila  malipo  katika shule tatu za Serikali  katika  kila  Wilaya  kwa  kipindi  cha   miaka  mitatu. Uwekezaji huo utakapokamilika utaleta mapinduzi makubwa ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini, jambo ambalo ni kichocheo kikubwa cha maendeleo.

89.         Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea na ujenzi wa Mikongo ya Mijini katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Dodoma kwa kushirikiana na watoa huduma za mawasiliano nchini. Aidha, itaanza Awamu ya Tano ya ujenzi wa Mkongo ambao utahusu kupeleka huduma kwa watumiaji wa mwisho (last mile connectivity) ambao ni pamoja na watu binafsi, Shule za Msingi, Sekondari na Vituo vya Afya ili kuwawezesha kutumia fursa za TEHAMA katika elimu mtandao, maktaba mtandao na afya mtandao.

 

HUDUMA ZA JAMII


Elimu

90.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imepata mafanikio makubwa katika Sekta ya Elimu kutokana na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Msingi na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari na pia kuingizwa kwa Sekta ya Elimu katika Mpango wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la Shule za Msingi za Serikali kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi Shule 16,538 mwaka 2015 na idadi ya Wanafunzi imeongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892 katika kipindi hicho. Vilevile, idadi ya Walimu wa Shule za Msingi imeongezeka kutoka Walimu 135,013 mwaka 2005 hadi Walimu 190,957 mwaka 2015 hatua ambayo imeimarisha uwiano wa Mwalimu kwa Mwanafunzi kutoka 1:56 mwaka 2005 hadi 1:43 mwaka 2015.

91.         Mheshimiwa Spika, katika Elimu ya Sekondari, idadi ya Shule za Sekondari za Serikali imeongezeka kutoka Shule 1,745 mwaka 2005 hadi Shule 4,753 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 172.4 Idadi ya Wanafunzi wa Shule za Sekondari wa Kidato cha Kwanza hadi cha Sita (6) imeongezeka kutoka Wanafunzi 524,325 mwaka 2005 hadi Wanafunzi 1,704,130 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 225. Idadi ya Walimu wa Sekondari pia imeongezeka kutoka 20,754 mwaka 2005 hadi Walimu 80,529 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 288. Pia kumekuwa na ongezeko la idadi ya vyumba vya madarasa kutoka 5,795 mwaka 2005 hadi 49,882 mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 760.8. Aidha, kufuatia Agizo la Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la kuboresha elimu ya sayansi nchini, ujenzi wa vyumba vya maabara  ya sayansi umeongezeka kwa kasi hadi kufikia  5,979 mwaka 2015 ikilinganishwa na 247 mwaka 2005, sawa na ongezeko la asilimia 2,321. Ongezeko hilo kubwa ni matokeo ya utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM. Nawapengeza sana Wananchi kwa kushirikiana vizuri na Serikali yao kufikia hatua hiyo.

92.         Mheshimiwa Spika, udahili katika Vyuo vya Elimu ya Ufundi na Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi umeongezeka kutoka Wanafunzi 78,586 mwaka 2005/2006 hadi kufikia Wanafunzi 145,511 mwaka 2013/2014, sawa na ongezeko la asilimia 85. Aidha, Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki vimeongezeka kutoka 23 mwaka 2005 hadi Vyuo Vikuu 49 mwaka 2013/2014. Pia, udahili katika Vyuo vya Elimu ya Juu umeongezeka kutoka Wanafunzi 40,719 mwaka 2005/2006 hadi Wanafunzi 204,175 mwaka 2013/2014. Wanafunzi wanaopata Mikopo ya Elimu ya Juu wameongezeka kutoka Wanafunzi 42,729 mwaka 2005/2006 hadi takriban Wanafunzi 94,000 mwaka 2013/2014. Mafanikio haya makubwa yametokana na utekelezaji madhubuti wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. Serikali itaendelea kuimarisha elimu katika ngazi zote kwa kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya Taifa na kufikia malengo ya nchi yetu ya kuwa na kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
                                                     

Afya                                                               

93.         Mheshimiwa Spika, Serikali ilianzisha Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) wa mwaka 2007 – 2017 ili kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wananchi wote. Chini ya Mpango huo, kila Kijiji kinatakiwa kuwa na Zahanati, kila Kata kuwa na Kituo cha Afya na kila Wilaya kuwa na Hospitali ya Wilaya. Kutokana na utekelezaji mzuri wa Mpango huo, idadi ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya nchini vimeongezeka kutoka Vituo 5,172 mwaka 2005 hadi 7,247 mwaka 2014 na Wataalamu 55,608 wa Kada ya Afya wamepangiwa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini katika kipindi hicho. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeajiri jumla ya Watumishi 8,119 ili kuongeza kasi ya utoaji huduma katika Sekta ya Afya. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuongeza idadi ya Vituo vya Kutolea Huduma za Afya, dawa na vifaa tiba pamoja na kuajiri Watumishi zaidi wa Sekta ya Afya.

94.         Mheshimiwa Spika, Serikali imeimarisha huduma za tiba za kibingwa katika Hospitali za Kanda, Hospitali Maalum na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kutoa huduma bora za afya na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi na matibabu. Huduma zilizoanzishwa nchini ni pamoja na upasuaji mkubwa wa moyo, upasuaji wa mgongo na ubongo, kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo na huduma ya mionzi. Hadi sasa, jumla ya wagonjwa 605 wamepatiwa huduma ya upasuaji mkubwa wa moyo na wagonjwa 1,198 walisafishwa damu katika hospitali hizo. 

95.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne, pia imepata mafanikio makubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Mpango Mkakati Mpya wa Kudhibiti Malaria Nchini na Mpango Mkakati wa Kuongeza Kasi ya Kupunguza Vifo Vitokanavyo na Uzazi na Vifo vya Watoto Wenye Umri chini ya miaka mitano. Kupitia Mpango wa Kudhibiti Malaria, jumla ya Vyandarua Milioni 40.7 vyenye Viuatilifu vya muda mrefu vilisambazwa nchini. Juhudi hizo pamoja na mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu na ongezeko la upatikanaji wa dawa mseto za malaria katika Vituo vyote vya Kutolea Huduma ya Afya nchini zimewezesha kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa watoto chini ya miaka mitano kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 9.5 mwaka 2012. Kupungua kwa maambukizi hayo pamoja na kuimarishwa huduma za chanjo kwa watoto na wajawazito kumechangia kupungua kwa vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 578 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi vifo 432 mwaka 2012. Vilevile, vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vimepungua kutoka vifo 112 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2005 hadi vifo 52 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2012. Juhudi hizo zimeiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano Barani Afrika ambazo zimepunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano kwa theluthi mbili na hivyo kuvuka Lengo Namba Nne la Malengo ya Milenia.

96.         Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua kubwa iliyofikiwa katika udhibiti wa magonjwa hapa nchini, tunakabiliwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani. Takwimu zinaonesha kuwa kila mwaka wanagundulika wagonjwa wapya wa saratani 44,000 na kati yao, wagonjwa 35,000 hufariki kutokana na ugonjwa huo. Hii ni changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa ipasavyo ili kuokoa maisha ya wananchi wetu. Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu ya utambuzi wa dalili za awali na umuhimu wa kuwahi kupata huduma. Hatua nyingine ni pamoja na kuimarisha Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kutoa matibabu na tiba shufaa kwa wagonjwa wa saratani. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani katika ngazi ya Kanda. Aidha, itaelimisha wananchi kutambua dalili za awali za saratani na umuhimu wa kuwahi Vituo vya Afya kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa saratani za aina mbalimbali zikiwemo saratani za matiti, shingo ya uzazi na tezi dume. Pia, Serikali itaimarisha huduma kwa wagonjwa wa saratani kwa kununua mashine za mionzi tiba ili kusogeza huduma karibu na wananchi na pia kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa wa saratani nje ya nchi.

 

Huduma kwa Wazee na Watu Wenye Ulemavu

97.         Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne inatambua kwamba watu wenye ulemavu wanayo haki ya kuthaminiwa utu wao, kuendelezwa, kuheshimiwa na kutobaguliwa. Pia, inatambua uwezo mkubwa walio nao katika kujiendeleza na kuchangia katika uchumi na maendeleo ya nchi yetu. Serikali pia inatambua mchango wa wazee na umuhimu wao kama hazina na chemchem ya busara katika jamii. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeendelea kuwapatia huduma muhimu wazee na watu wenye ulemavu kupitia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Wazee na Sheria ya Usimamizi ya Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2010. Pia, Serikali imepanua na kuimarisha fursa ya ushiriki wa walemavu katika siasa na uendeshaji wa uchumi pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa walemavu. Aidha, imeimarisha upatikanaji wa huduma za msingi kama vile elimu, afya, mikopo na ujenzi wa majengo ya umma yanayozingatia mahitaji maalum ya watu wenye ulemavu.

98.         Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa jamii na kupiga vita mila na desturi ambazo hazitoi fursa katika kulinda utu, ushiriki, ulinzi na maendeleo ya watu wenye ulemavu na wazee. Natoa wito kwa jamii kuwa na moyo wa kuwasaidia na kuwatunza wazee na watu wenye ulemavu. Vilevile, jamii haina budi kuondokana na mila potofu zinazoathiri upatikanaji haki na maslahi ya wazee na watu wenye ulemavu kama ilivyo kwa makundi mengine. Katika kipindi kijacho, Serikali ya CCM itaweka mkazo zaidi katika kuhudumia wazee na watu wenye ulemavu kwa kuwapatia huduma stahiki na fursa zitakazoweza kuinua hali zao za maisha.

Lishe

99.         Mheshimiwa Spika, matokeo ya utafiti wa Hali ya Afya nchini uliofanyika mwaka 2010 yalionesha kwamba hali ya lishe nchini siyo ya kuridhisha, hususan kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano (5). Vilevile, utafiti huo ulibaini kuwa hali ya lishe ya wanawake walio kwenye umri wa kuzaa siyo ya kuridhisha kwa kuwa zaidi ya nusu ya wanawake hao wana upungufu wa damu na mmoja kati ya 10 wana lishe duni. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2011/2012 hadi 2015/2016 ambao niliuzindua tarehe 19 Septemba, 2011. Ili kutekeleza Mkakati huo, Serikali iliunda Kamati ya Kitaifa ya Lishe yenye jukumu la kusimamia na kuratibu masuala yote ya lishe nchini.  Pia, Serikali imeanzisha Dawati la Lishe katika Wizara zinazojishughulisha na masuala ya lishe na katika Halmashauri zote nchini. Aidha, Wizara ya Fedha imetoa Kasma maalum kwa ajili ya Halmashauri kutenga fedha za lishe. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuendelea kusimamia utekekelezaji wa Kanuni za Kusindika Chakula kwa Kuongeza Virutubishi.

100.      Mheshimiwa Spika, kutokana na jitihada hizo, Tathimini ya Kitaifa ya Hali ya Lishe Nchini iliyofanyika mwaka 2014 imeonesha kuwa hali ya lishe kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano imeanza kuimarika. Takwimu zinaonesha kuwa kiwango cha udumavu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 42 mwaka 2010 hadi asilimia 34.7 mwaka 2014, ukondefu umeshuka kutoka asilimia 4.9 hadi asilimia 3.8 na  uzito pungufu umeshuka kutoka asilimia 16.2 mwaka 2010 hadi asilimia 13.4 mwaka 2014.

101.      Mheshimiwa Spika, pamoja na matokeo hayo ya kutia moyo, hasa ya kushuka kwa kiwango cha udumavu Kitaifa, bado kuna Mikoa tisa ya Tanzania Bara ambayo ina viwango vya zaidi ya asilimia 40 ya watoto waliodumaa. Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe, Kagera, Dodoma, Ruvuma, Rukwa, Kigoma, Katavi na Geita. Matokeo hayo yamebainisha pia kupungua kwa matumizi ya chumvi yenye madini joto katika Kaya kutoka asilimia 81.7 mwaka 2010 hadi asilimia 64.4 mwaka 2014. Hii siyo habari njema ikizingatiwa kwamba upungufu wa madini joto una madhara makubwa ikiwemo tatizo la tezi ya shingo na watoto kuvia kiakili.  Ili kukabiliana na hali hiyo, Mamlaka za Udhibiti zikiwezo Mamlaka ya Chakula na Dawa na Shirika la Viwango Tanzania zimeagizwa zihakikishe kwamba chumvi inayozalishwa na kuuzwa nchini imeongezewa madini joto kwa viwango vinavyokubalika kimataifa. Aidha, ninatoa wito kwa jamii kuhakikisha kuwa zinapata chakula chenye lishe bora na kutumia chumvi yenye madini joto. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itakamilisha Sera ya Taifa ya Lishe na kuandaa Mpango wa Utekelezaji utakaonesha gharama na jukumu la kila mdau katika kupambana na tatizo la lishe duni.                                     

Maji
102.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa Mkakati wa Kuendeleza Sekta ya Maji na Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Ili kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji nchini, Sekta ya Maji ilijumuishwa katika Mpango wa Tekeleza Sasa kwa Matokeo Makubwa. Kutokana na utekelezaji mzuri wa programu na miradi ya maji, mafanikio makubwa yamepatikana Mjini na Vijijini. Hadi mwezi Februari 2015, miradi ya maji ya Vijiji 931 ilikamilika ikilinganishwa na miradi 248 iliyotekelezwa mwaka 2013/2014. Aidha, miradi mingine katika Vijiji 607 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza upatikanaji wa huduma za maji Vijijini hadi kufikia asilimia 53 ambapo jumla ya watu milioni 19.9 wamenufaika ikilinganishwa na watu 2,390,000 walionufaika na huduma hiyo Desemba, 2013. Katika mwaka 2015/2016, Serikali imepanga kujenga miradi ya maji 731 katika Vijiji 1,189 na kujenga Vituo vya kuchotea maji 25,790 ambavyo vitanufaisha takribani watu milioni saba (7). Kukamilika kwa miradi hiyo kutawezesha upatikanaji wa huduma ya maji Vijijini kufikia asilimia 71.

103.      Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza wastani wa upatikanaji wa huduma ya maji katika Miji Mikuu ya Mikoa kutoka asilimia 78 mwaka 2005 hadi asilimia 86 mwezi Desemba, 2014. Aidha, kupitia Mpango wa Kuboresha Huduma ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam, hadi Januari, 2015 Serikali imekamilisha mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini. Vilevile, imekamilisha ulazaji wa kilomita 53 za bomba kuu kutoka mtambo wa maji wa Ruvu Chini hadi matanki ya Chuo Kikuu cha Ardhi, sawa na asilimia 94 ya urefu wa bomba lote. mradi huo utakapokamilika utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 180 hadi lita milioni 270 kwa siku. Serikali pia imeendelea kutekeleza mradi wa upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Juu ambao unahusisha upanuzi na ulazaji wa bomba kuu  kutoka kwenye  mtambo huo hadi Kibamba na ujenzi wa tanki jipya la Kibamba. Mradi huo utakapokamilika, utaongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 82 hadi lita milioni 196 kwa siku. Katika mwaka 2015/2016, Serikali itakamilisha utekelezaji wa mradi huo.

MAENEO MAPYA YA UTAWALA

104.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imeendelea na jitihada za kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kuanzisha maeneo mapya ya utawala katika ngazi mbalimbali. Katika kipindi hiki, Serikali imeanzisha Mikoa mipya minne ya Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Aidha, imeanzisha Wilaya mpya 19, Halmashauri mpya 36 na Mamlaka za Miji Midogo mpya 12. Pia, Serikali imeanzisha Kata 497 na hivyo kuongeza idadi ya Kata zilizopo nchini kutoka Kata 3,337 mwaka 2005 hadi 3,834 mwaka 2015. Vilevile, Serikali imeongeza Vijiji kutoka 11,795 hadi Vijiji 12,300 na Mitaa kutoka 2,995 hadi 3,939. Idadi ya Vitongoji nchini nayo imeongezeka kutoka 60,359 hadi kufikia 64,691 katika kipindi hicho. Ni imani yangu kwamba kuanzishwa kwa maeneo hayo kutawawezesha Wananchi kupata huduma muhimu za kiutawala na za kijamii kwa ufanisi zaidi karibu na maeneo wanayoishi.

USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA

105.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imejenga barabara za lami zenye urefu wa Kilometa 47.7 na kuboresha huduma ya umeme, maji safi na majitaka katika Mji wa Dodoma. Aidha, imeandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi, ramani za makazi na maeneo ya uwekezaji kulingana na kasi ya maendeleo ya Mji. Vilevile, imeboresha na kuhalalisha maeneo yaliyojengwa kiholela. Kuanzia mwaka 2005 hadi 2014, jumla ya viwanja 20,394 vimepimwa na kumilikishwa kwa waendelezaji na vibali vya ujenzi wa nyumba 2,869 vimetolewa. Katika  mwaka 2015/16, Serikali imepanga kusanifu miundombinu ya barabara zenye urefu wa kilometa 55 na mitaro ya maji ya mvua yenye urefu wa kilometa 13 pamoja na kujenga barabara zenye urefu wa kilometa tisa (9) kwa kiwango cha lami na Kilometa saba (7) kiwango cha changarawe. Pia, Serikali itapima Viwanja 3,786 na kuandaa Hatimiliki 1,200 za viwanja.

USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

106.      Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kujenga mahusiano ya kirafiki na ushirikiano wa kiuchumi na nchi na vyombo mbalimbali vya Kikanda na Kimataifa unaozingatia maslahi makubwa ya Taifa letu. Mafanikio makubwa yamehusishwa na ziara za Viongozi wa Kitaifa katika nchi mbalimbali ambazo zimeimarisha ushirikiano kati ya nchi yetu na nchi hizo. Ziara hizo pia zimechochea na kukuza biashara, utalii na kuvutia uwekezaji. Vilevile, ziara hizo zimekuwa chachu kwa Viongozi wengi wa Nchi na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa na Kikanda kutembelea Tanzania wakiwemo Viongozi wa Mataifa makubwa ya China, Marekani, Ujerumani, Japan na Uingereza. Ziara zilizofanywa na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimeleta mafanikio makubwa hasa kuvutia wawekezaji katika Sekta za Miundombinu ya barabara na uchukuzi, nishati, gesi asilia, elimu, afya, maji na maliasili na utalii.

107.      Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza diplomasia ya kiuchumi, Serikali inatumia Balozi zake kuitangaza nchi ili kuvutia wawekezaji, kutangaza vivutio vya utalii na kutafuta fursa za masoko ndani na nje ya nchi. Sambamba na hatua hizo, Serikali imeendelea kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanapata fursa za kuchangia maendeleo ya nchi yao. Mwezi Agosti 2014, Serikali iliandaa Mkutano wa Kwanza wa ‘Diaspora’ uliofanyika Dar es Salaam kwa lengo la kuwakutanisha pamoja Watanzania waishio nje ya nchi ili kujadili namna wanavyoweza kuchangia kukuza uchumi wetu kulingana na fursa zinazopatikana nje ya nchi. Serikali itaendelea kuwashirikisha Watanzania waishio nje ya nchi kwenye shughuli za maendeleo ili waweze kutoa mchango mkubwa kwa Taifa kwa kutumia fursa na uzoefu wanaopata kwenye nchi wanazoishi.
                 
108.      Mheshimiwa Spika, nchi yetu inashiriki kikamilifu katika kuimarisha ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mtangamano wa Afrika Mashariki unahusisha hatua zifuatazo: Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa. Katika hatua ya kwanza, Tanzania imefanikiwa kukuza biashara kati yake na nchi wanachama kutokana na kuondolewa kwa ushuru wa forodha. Hatua hiyo imesaidia Tanzania kuongeza mauzo ya bidhaa zake katika Nchi Wanachama. Mfano, katika mwaka 2013, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 1,120 na imenunua bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 397. Katika hatua ya pili ambayo ni Soko la Pamoja la Afrika Mashariki, Tanzania imefungua fursa za uwekezaji na ajira hasa katika Sekta zinazokabiliwa na uhaba wa Wataalam kama vile Wahadhiri wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Walimu wa Shule za Sekondari katika fani ya hisabati, fizikia, baiolojia na kemia.

109.      Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2013 Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki walitia saini Itifaki ya Umoja wa Fedha ambayo ni hatua ya tatu ya Mtangamano. Kwa sasa nchi wanachama zinatekeleza Mpango Kazi wa Miaka Kumi wa Kuelekea kwenye Eneo Huru la Sarafu Moja ifikapo mwaka 2024.  Katika Mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuratibu utekelezaji wa Himaya Moja ya Forodha; Mpango Kazi wa Miaka Kumi wa Kuelekea Sarafu Moja; na kuongeza kasi ya kuondoa vikwazo visivyo vya kiushuru katika biashara baina ya nchi wanachama.

MASUALA MTAMBUKA   

                                                           

Jinsia

110.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne inatambua uwezo na nguvu kubwa ya wanawake katika kusukuma kasi ya maendeleo na kuleta mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Kwa msingi huo, Serikali imeongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi wa kisiasa na nafasi za maamuzi. Katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne, idadi ya Mawaziri wanawake imeongezeka kutoka 6 kati ya Mawaziri 25 katika mwaka 2005 hadi kufikia 10 kati ya Mawaziri 30 mwaka 2015; Wakuu wa Mikoa wameongezeka kutoka 2 kati ya Wakuu wa Mikoa 21 mwaka 2005 hadi 7 kati ya Wakuu wa Mikoa 25 mwaka 2015; Wakuu wa Wilaya wanawake wameongezeka kutoka  wanawake 20 kati ya Wakuu wa Wilaya 104 mwaka 2005 hadi kufikia Wakuu wa Wilaya wanawake 46 kati ya Wakuu wa Wilaya 133 mwaka 2015. Majaji wanawake wameongezeka kutoka 8 kati ya 50 mwaka 2005 hadi kufikia 24 kati ya Majaji 67  mwaka 2015;  na Wabunge Wanawake wameongezeka kutoka 62 kati ya Wabunge 288 mwaka 2005 hadi kufikia 127 kati Wabunge 357 mwaka 2015.

111.      Mheshimiwa Spika, pia, Serikali imeendelea kuwahamasisha wanawake kujiendeleza kielimu na kujenga uelewa wao katika kuweka nguvu za kutetea haki zao na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kimaendeleo. Vilevile, Serikali imewajengea uwezo wa ujasiriamali, utaalam wa biashara, jinsi ya kupata mitaji zaidi, masoko pamoja na kutoa mikopo mbalimbali. Idadi ya wanawake waliopata mikopo kupitia Benki ya Wanawake Tanzania imeongezeka kutoka wanawake wajasiriamali 689 mwaka 2010 hadi kufikia 42,648 mwaka 2014.

Vita Dhidi ya Rushwa

112.      Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na mapambano dhidi ya rushwa kwa kutekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti Rushwa Nchini (NACSAP). Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeendelea kushughulikia uchunguzi wa tuhuma 3,311 za rushwa ambapo uchunguzi wa tuhuma 528 ulikamilika. Vilevile, majalada 187 ya rushwa zilizotokana na Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yalichunguzwa na kati ya hayo 31 yalikamilika na kuombewa kibali cha mashtaka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka, na tisa (9) yalipata kibali cha kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani. Ili kuimarisha udhibiti wa Rushwa, Serikali imeandaa Mkakati wa Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, kwa kushirikisha Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Pia, Serikali imeandaa rasimu ya Muswada wa Mapendekezo ya Marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

113.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, TAKUKURU itaendelea kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa, kuwafikisha watuhumiwa mbele ya Vyombo vya Sheria na kuishauri Serikali namna ya kuziba mianya ya rushwa. Aidha, itachunguza tuhuma 2,783 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na kukamilisha chunguzi za tuhuma kumi (10) za rushwa kubwa na kuendesha Kesi 659 zilizopo Mahakamani na zitakazoendelea kufunguliwa, na pia kutoa elimu kuhusu rushwa kwa Wananchi.
                             

Hifadhi ya Mazingira

114.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Wananchi imeendelea na juhudi za kupambana na uharibifu wa  mazingira  kwa kuchukua hatua mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kusimamia sheria zinazozuia ukataji miti kiholela na uchomaji moto na kuharibu vyanzo vya maji; kuweka mazingira safi Mijini na Vijijini pamoja na kuhimiza na kusimamia zoezi la upandaji miti kila mwaka ambapo kati ya mwaka 2006 na 2013, jumla ya miti bilioni 1.3 ilipandwa. Vilevile, Serikali imeandaa na kutekeleza Mpango wa Kudhibiti Hewa Ukaa na Mabadiliko ya Tabia Nchi. Aidha, Serikali inatekeleza Mkakati Maalum wa Kuhifadhi Mazingira katika Mito, Bahari, Maziwa na Ukanda wa Pwani. Hatua hizo zimeleta mwamko wa Wananchi wengi kuhifadhi mazingira. Napenda kuchukua fursa hii kuipongeza Mikoa na Halmashauri ambazo zimefanya juhudi kubwa kuhimiza na kusimamia masuala ya hifadhi ya mazingira na usafi katika maeneo yao. 

115.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, Serikali imeimarisha ukaguzi wa athari za mazingira kwa kukagua Viwanda na Taasisi 30 pamoja na Migodi 13. Katika ukaguzi huo, jumla ya viwanda 11 vya Mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro vilivyobainika kuchafua mazingira vilipewa notisi ya kurekebisha mifumo ya majitaka na uchafuzi hewa. Vilevile, Viwanda 19 vya Mikoa ya Kanda ya Ziwa,  Dar es Salaam na  Mtwara vimetozwa faini kwa kukiuka Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004. Ukaguzi unaendelea katika maeneo mengine nchini na wale watakaobanika kukiuka Sheria ya Mazingira watachukuliwa hatua stahiki. Naagiza Viongozi katika ngazi zote kushirikiana na Wananchi kusimamia suala la kutunza na kuhifadhi mazingira katika maeneo yao.
                 

Menejimenti ya Maafa

116.      Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na maafa mbalimbali katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Maafa hayo ni pamoja na mafuriko, ukame, maporomoko ya udongo na migodi ya wachimbaji wadogo, kuporomoka kwa majengo, milipuko ya mabomu, radi, mvua ya mawe iliyoambatana na upepo mkali na ajali za barabarani na majini. Serikali ya Awamu ya Nne kwa kushirikiana na wadau imefanya jitihada za kukabiliana na maafa hayo kwa kuwapatia waathirika huduma za msingi kama vile chakula, maji, matibabu, makazi ya muda, msaada wa maziko kwa waliofiwa na fidia kwa uharibifu wa nyumba na samani.  

117.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2014, Serikali ilitoa jumla ya tani 336,378 za chakula zenye thamani ya Shilingi Bilioni 128.2 na Shilingi Bilioni 24.2 za usafiri kwa ajili ya kukabiliana na uhaba wa chakula katika maeneo mbalimbali nchini. Pamoja na msaada wa chakula, Serikali ilitumia Shilingi Bilioni 25.7 kulipa fidia na kifuta machozi kwa wananchi walioathirika na maafa mbalimbali yakiwemo ya mlipuko wa mabomu Mbagala na Gongolamboto Jijiji Dar es Salaam. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kukabiliana na maafa nchini kwa kutoa mafunzo ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya pamoja na vikosi vya Majeshi. Vilevile, Serikali imehakikisha kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya  Chakula umehifadhi chakula cha kutosha wakati wote. Katika mwaka 2014/2015, Sheria ya Menejimenti ya Maafa ilitungwa na Bunge ili kuongeza ufanisi katika kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali ya kawaida baada ya maafa kutokea. Sheria hiyo pia imeweka utaratibu wa kuanzisha Wakala wa Menejimenti ya Maafa pamoja na kuunda Kituo cha Utendaji na Mawasiliano wakati wa Dharura. Serikali inakamilisha Kanuni za Sheria hiyo ili kurahisisha matumizi na usimamizi wa Sheria hiyo.

118.      Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hali ya Hewa ilitoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa upungufu wa mvua za vuli na masika. Kwa kuzingatia tahadhari hiyo, mwezi Januari 2015, Serikali ilifanya tathmini ya hali ya chakula nchini. Tathmini hiyo ilibaini kwamba, Halmashauri za Wilaya 23 katika Mikoa 12 zimeonesha dalili ya upungufu wa chakula kutokana na mvua kidogo za vuli. Tathmini inaonesha kuwa zaidi ya watu 400,000 watakabiliwa na upungufu wa chakula. Serikali imetenga tani 10,000 za chakula cha msaada kwa wananchi hao na tani 294.3 za mbegu bora za mazao mbalimbali zinazokomaa katika muda mfupi. Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na  Mikoa, Wilaya na Halmashauri  zinaendelea kufanya tathmini nyingine ya hali ya chakula nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi za Wananchi wenye upungufu wa chakula ili wapatiwe chakula kwa wakati.

119.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2015/2016, Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wake katika Menejimenti ya Maafa kwa kutoa elimu kwa wadau, na kuanza maandalizi ya kuanzisha Wakala wa Menejimenti ya Maafa kama ilivyoainishwa na Sheria ya Menejimenti ya Maafa ya mwaka 2014.

Udhibiti wa UKIMWI

120.      Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne imeendeleza jitihada za kupambana na ugonjwa wa UKIMWI ambao umekuwa tishio kubwa kwa maendeleo ya Taifa letu. Serikali imetekeleza Mkakati wa Taifa wa Pili na wa Tatu wa Kudhibiti UKIMWI na kuanza maandalizi ya Sera Mpya ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI. Mabaraza 92 ya Wilaya ya Watu Waishio na Virusi vya UKIMWI yameundwa kwa lengo la kulinda na kutetea maslahi yao na kufanya uraghabishi ili kuongeza mwitikio wa jamii katika udhibiti wa VVU na UKIMWI. Vilevile, Serikali inatekeleza Mpango wa Matunzo na Matibabu kwa Waishio na Virusi vya UKIMWI ambapo vituo vinavyotoa huduma hiyo vimeongezeka kutoka Vituo 700 vilivyokuwepo mwaka 2008 hadi kufikia Vituo 1,209 mwaka 2014. Katika kipindi hicho, idadi ya watu waliosajiliwa katika Mpango huo imeongezeka kutoka 403,378 hadi milioni 2.2 na kati yao, waathirika 850,274 wanapata huduma za tiba na matunzo katika Vituo vya Afya kote nchini. Katika mwaka 2014/2015, Serikali imeanzisha Mfuko wa Kudhibiti UKIMWI kwa lengo la kuhakikisha kuwa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya udhibiti wa UKIMWI unakuwa endelevu.

121.      Mheshimiwa Spika, wanawake wajawazito 75,866 waishio na VVU walipata huduma ya dawa za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kutoa elimu ya VVU na UKIMWI kwa jamii na kuhamasisha upimaji wa hiari wa afya na tohara ya hiari ya kitabibu kwa wanaume ambapo hadi mwaka 2014, jumla ya wanaume 676,225 wamepatiwa huduma hiyo. Kutokana na juhudi hizo, utafiti uliofanyika mwaka 2011/2012 umeonesha kuwa kiwango cha ushamiri wa Virusi vya UKIMWI kwenye jamii kimepungua kutoka asilimia 7.0 mwaka 2003/2004 hadi asilimia 5.7 mwaka 2007/2008 na asilimia 5.1 mwaka 2011/2012. Maambukizi mapya yamepungua kutoka wastani wa watu 140,000 mwaka 2009 hadi 74,000 mwaka 2014 na maambukizi mapya kwenye rika la watoto wa umri wa miaka 0 hadi 14 yamepungua kutoka 33,000 hadi 17,000 mwaka 2013. Hii inaashiria kupungua kiwango cha maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kipindi hicho. Vilevile, vifo vitokanavyo na UKIMWI vimepungua kutoka 145,000 mwaka 2005 hadi 80,000 mwaka 2013.

122.      Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2015/2016, itaimarisha mapambano dhidi ya maambukizi ya UKIMWI, hususan kwa Vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24, kupunguza kasi ya maambukizi kwenye Mikoa 12 yenye mzigo mkubwa wa ugonjwa wa UKIMWI, kukamilisha maandalizi  ya  taratibu  za uendeshaji wa Mfuko wa Kudhibiti UKIMWI, na kutoa elimu kuhusu VVU na UKIMWI. Aidha, kuendelea kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa kwenye Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI. Serikali kwa kushirikiana na wadau itafanya Utafiti wa nne wa Kutambua Kiwango cha Maambukizi kwa kila Mkoa.
             

Udhibiti wa Dawa za Kulevya

123.      Mheshimiwa Spika, matumizi ya Dawa za Kulevya ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wananchi wetu na kuathiri afya za watumiaji ambao wengi wao ni vijana na kudhoofisha nguvu kazi na uchumi wa Taifa letu. Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo.  Hatua  hizo  ni  pamoja  na kuimarisha uwezo wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Nchini, kuanzisha Kikosi Kazi cha Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kutekeleza programu mbalimbali za uelimishaji Vijana juu ya athari za matumizi na biashara ya Dawa za Kulevya. Aidha, huduma za matibabu ya dawa ya Methadone kwa wanaotumia dawa za kulevya aina ya Heroin zimeanzishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Mwananyamala na Temeke ambapo hadi Machi 2015 watumiaji 2,223 walikuwa wakipata huduma za matibabu. Vilevile, suala la dawa za kulevya limeingizwa kwenye mitaala ya Shule za Msingi. Serikali pia inajenga Kituo cha Waathirika wa Dawa za Kulevya katika Hospitali ya Rufaa ya Mirembe, Dodoma.

124.      Mheshimiwa Spika, operesheni zilizoendeshwa na Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya kuanzia mwezi Julai 2014 hadi Machi 2015, zimewezesha kukamatwa kwa kilo 126.4 za dawa za kulevya aina ya Heroin,  kilo 1.8 za Cocaine na kilo 8,210 za bangi. Jumla ya watuhumiwa 39 wamekamatwa na kufikishwa kwenye Vyombo vya Sheria. Katika kipindi hicho, Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ilitoa elimu kwa umma wakiwemo waandishi wa habari, wasanii na Wanafunzi wa Shule za Sekondari na Vyuo Vikuu. Pia, katika mwaka 2014/2015 Sheria Mpya ya Kudhibiti Dawa za Kulevya ilitungwa na Bunge lako Tukufu ili kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya nchini.

125.      Mheshimiwa Spika, Serikali kwa mwaka 2015/2016, itaimarisha utoaji wa elimu kwa umma juu ya athari za biashara na matumizi ya dawa za kulevya na kukijengea uwezo zaidi Kikosi Kazi cha Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini. Serikali pia itakamilisha Kanuni za utekelezaji wa Sheria Mpya ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya na kuendeleza ushirikiano na nchi nyingine katika mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya.
                                                                                         

HITIMISHO

126.      Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwa muhtasari baadhi ya shughuli ambazo Serikali ya Awamu ya Nne imetekeleza kwa kipindi cha miaka kumi. Aidha, nimetoa mwelekeo wa kazi zitakazofanyika katika mwaka 2015/2016. Ningependa kusisitiza mambo muhimu yafuatayo:

(a)          Ili Nchi yetu iendelee, ni lazima tukuze Uchumi kwa kuongeza Uzalishaji na Tija katika Sekta zote. Tunahitaji kutoa kipaumbele zaidi katika Sekta ya Kilimo kwa maana ya uzalishaji wa  mazao ya chakula na biashara, ufugaji, uvuvi na matumizi  sahihi ya misitu yetu. Hii ni kwa sababu zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea Kilimo.

Kwa hiyo, Azma ya “Kilimo Kwanza” iwe ni kichocheo cha kuhimiza mipango na mikakati tuliyojiwekea ya kuendeleza Kilimo katika Nchi yetu. Natoa wito kwa Viongozi na Wadau wa Maendeleo kushirikiana na Serikali kuwahimiza Wananchi kuhusu matumizi ya teknolojia sahihi ikiwemo mbolea, dawa za kuua wadudu, mbegu bora na zana za kisasa za  kilimo  ili  kuongeza  uzalishaji  katika  kilimo na kukibadili kutoka kilimo cha kujikimu kuwa chenye tija na cha kibiashara. Pia, tuwahimize kuhusu umuhimu wa kutumia wataalamu wa kilimo waliopo katika maeneo yao. Serikali itaweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji kutoka Sekta Binafsi, kuimarisha masoko pamoja na utafiti na kuhimiza Kilimo cha Umwagiliaji, ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao na kuweka utaratibu madhubuti wa mikopo.

(b)          Tumeona mafanikio yaliyopatikana kwa kutekeleza Awamu ya Pili ya MKUKUTA iliyoanza Julai, 2010 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Aidha, tumeshuhudia kuongezeka kwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya kipaumbele chini ya mfumo wa BRN! Matokeo ya utekelezaji wa mfumo huo ni mazuri na yanatia matumaini na inabidi tuendelee kufuatilia kwa karibu miradi ya kipaumbele na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kupima matokeo. Nawaomba tuendeleze mafanikio yaliyopatikana ili kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea. Pia, hatuna budi kutumia rasilimali adimu tulizonazo kwa umakini na uangalifu mkubwa ili kufikia malengo hayo.

(c)          Tumefanya kazi nzuri ya kujenga madarasa ya Shule za Sekondari kwa ajili ya Wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba. Kila Mamlaka ya Serikali za Mitaa ijipange vizuri kuhakikisha kwamba Wanafunzi wote wanaofaulu wanapata nafasi  ya  kujiunga na kidato cha kwanza. Aidha, ujenzi wa madarasa uende sambamba na ujenzi wa nyumba za Walimu, maabara, maktaba, hosteli na vyoo vya kutosha. Nazihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa nyumba za Walimu, maabara na hosteli za Wanafunzi ili kupanua na kuimarisha miundombinu ya Shule nchini.

(d)          Ardhi  tuliyonayo  ni hazina kubwa inayohitaji kuwa na Mpango wa Matumizi Bora. Hivyo, nazihimiza  Mamlaka  za Serikali za Mitaa kuandaa na kutekeleza  kwa kasi mipango ya matumizi bora ya ardhi katika maeneo yao ikiwemo kupima vijiji, mashamba na viwanja. Aidha, nawakumbusha Wananchi kutii Sheria, Kanuni na Taratibu za Ardhi zilizopo ili kuepuka migogoro ya ardhi hasa ile ya wafugaji na wakulima; wananchi na wawekezaji; na wafugaji/wakulima na maeneo ya Hifadhi.

(e)          Tunayo  changamoto  ya kuyasaidia makundi maalum  katika jamii yetu kama vile Watu wenye Ulemavu wa Ngozi na vikongwe ambao bado wanaendelea kuuawa kikatili. Tuendelee kushirikiana kumaliza kabisa tatizo hilo kwa kuwafichua wale wanaofanya vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria. Naomba tusichoke kuwasaidia Watu wenye Ulemavu kwa kuwapa moyo, kuwaondolea hofu, na kuwasaidia pale inapobidi ili waweze kujiletea maendeleo.

(f)           Tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi Oktoba, 2015. Serikali itahakikisha amani, utulivu na umoja katika nchi yetu unadumishwa. Natoa wito kwa wale wote watakaogombea nafasi mbalimbali za Uongozi na Wananchi wote kuepuka kujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa uteuzi, kampeni na Uchaguzi Mkuu. Aidha, Viongozi wa Vyama vya Siasa na Wanachama wao wanadi Sera na mikakati ya Vyama vyao kwa kutumia lugha ya kistaarabu badala ya kutumia lugha zisizo na staha zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu nchini. Tujenge Taifa moja lenye msingi wa kuheshimiana na kuenzi amani na utulivu uliopo nchini.

127.      Mheshimiwa Spika, kabla ya kuhitimisha hoja yangu, nimwombe Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa atoe  maelezo ya Mapitio ya Kazi Zilizofanyika katika Mwaka 2014/2015 na Mwelekeo  wa Kazi za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2015/2016. Ni matumaini yangu kwamba maelezo hayo yatawezesha Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kufahamu kwa upana shughuli zinazotekelezwa na Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

 

SHUKRANI

128.      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii sasa kuwashukuru timu nzima ya Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushauri wao ambao umewawezesha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kutekeleza majukumu yao ya Kitaifa kwa ufanisi katika kipindi cha Miaka Mitano iliyopita. Aidha, niwashukuru wafanyakazi wote wa Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Yohana Sefue pamoja na vyombo vyote vya dola kwa kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo na kukamilisha maandalizi  yote ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2015/2016, pamoja  na  Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya kila Wizara, Mikoa, Wakala na Taasisi za Serikali Zinazojitegemea. Ninawashukuru Watanzania wote na Washirika wa Maendeleo kwa michango yao ambayo imewezesha Serikali kufanikisha kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

129.       Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Mhandisi Christopher Kajoro Chiza, Mbunge wa Buyungu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Uwekezaji na Uwezeshaji) ; Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi (Sera, Uratibu na Bunge) ; Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara Vijijini, Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ; Mheshimiwa  Aggrey  Joshua  Mwanri,  Mbunge  wa  Siha, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mheshimiwa Majaliwa Kassim Majaliwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) kwa msaada mkubwa na ushirikiano walionipa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Shukrani za pekee kwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa jitihada walizoonesha katika kipindi hiki. Ninawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Florens M. Turuka na Bwana Jumanne A. Sagini na Naibu Makatibu Wakuu, Bibi Regina L. Kikuli na Bwana Kagyabukama E. Kiliba, Bwana Zuberi M. Samataba na Dkt. Deo M. Mtasiwa, kwa ushauri wao wa kitaalam ambao wamenipa mimi na  Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki. Ninawashukuru kwa kukamilisha maandalizi yote ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2015/2016.

130.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2014/2015, nchi yetu imepata Misaada na Mikopo kutoka kwa Wahisani mbalimbali. Misaada na Mikopo hiyo imetoka kwa Nchi Rafiki, Nchi Wahisani, Taasisi za Fedha Duniani, Mashirika ya Umoja wa Mataifa, Mifuko mbalimbali ya Fedha Duniani,  Madhehebu  ya  Dini,  Mashirika Yasiyo ya Serikali, Mashirika ya Umma na Kampuni Binafsi za ndani. Misaada na Mikopo hiyo imechangia sana katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ninapenda kuwashukuru wote kwa dhati na kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini Misaada na Mikopo waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za kuleta maendeleo ya Taifa letu.

131.      Mheshimiwa Spika, ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa Jimbo la Katavi kwa imani na heshima kubwa waliyonipa ya kunichagua kuwa Mbunge wao tangu mwaka 2000. Aidha, ninawashukuru Viongozi wenzangu wote na Wananchi wote kwa ushirikiano wa dhati  walionipa katika kipindi chote cha uongozi wangu. Kipekee, ninapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kubwa kwangu  kuniteua kuwa Waziri Mkuu kwa vipindi viwili tangu tarehe 8 Februari, 2008. Ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake makini alioutoa kwangu na pia kwa kufanya  kazi naye kwa karibu na kwa upendo mkubwa na hivyo kuniwezesha kujifunza mengi kutoka kwake katika kipindi hiki. Ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano walionipa ambao umeniwezesha kuwatumikia Watanzania katika nafasi hii kwa takriban Miaka Saba na Miezi Saba!

132.      Mheshimiwa Spika, vilevile, ninawashukuru viongozi wenzangu  wote wa kitaifa na viongozi wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano ambao umeniwezesha kutekeleza jukumu kubwa la kusimamia Utendaji wa Serikali katika Sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Nirudie tena kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mkubwa mlionipa katika kipindi changu cha kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni. Nasema Asanteni sana!

133.      Mheshimiwa Spika, mwisho ningependa kutoa shukrani kwa familia yangu, Mama Tunu Pinda na watoto wote kwa uvumilivu wao mkubwa na kuniombea pamoja na kutia moyo jambo ambalo limeniwezesha kutekeleza majukumu yangu ipasavyo.

MAKADIRIO YA  MATUMIZI  YA  FEDHA  YA OFISI  YA  WAZIRI MKUU, OFISI  YA  WAZIRI MKUU - TAWALA  ZA  MIKOA  NA  SERIKALI ZA MITAA NA OFISI YA BUNGE YA MWAKA 2015/2016


134.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2015/2016, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu kuidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni Mia Tatu Kumi na Moja, Milioni Mia Saba Sitini na Tatu, Mia Sita Themanini na Moja Elfu (311,763,681,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Sitini na Nne, Milioni Mia Nne Themanini, Mia Tatu na Sabini na Saba Elfu (264,480,377,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Arobaini na Saba, Milioni Mia Mbili na Themanini na Tatu, Mia Tatu na Nne Elfu (47,283,304,000) ni za Miradi ya Maendeleo.

135.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Taasisi zake inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Nne na Tano, Milioni Mia Moja na Moja, Mia Moja Tisini na Tano Elfu (405,101,195,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Hamsini, Milioni Mia Tano na Thelathini na Tano, Mia Tano Sitini na Tisa Elfu (50,535,569,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Tatu Hamsini na Nne, Milioni Mia Tano Sitini na Tano, Mia Sita Ishirini na Sita Elfu (354,565,626,000) ni za Miradi ya Maendeleo.

136.       Mheshimiwa Spika, Ofisi za Wakuu wa Mikoa zinaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili na Themanini, Milioni Mia Mbili Kumi na Nane, Mia Sita Sitini na Moja Elfu (280,218,661,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Mia Mbili Ishirini na Tisa, Milioni Mia Tatu Kumi na Tatu, na Sabini Mbili Elfu (229,313,072,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Hamsini, Milioni Mia Tisa na Tano, Mia Tano Themanini na Tisa Elfu (50,905,589,000) ni za Miradi ya Maendeleo. Halmashauri zote zinaombewa jumla ya Shilingi Trilioni Nne, Bilioni Mia Saba Sitini na Sita, Milioni Mia Saba, Mia Tano Thelathini na Tatu Elfu (4,766,700,533,000). Kati ya fedha hizo, Shilingi Trilioni Nne, na Bilioni Ishirini na Tatu, Milioni Mia Mbili Hamsini na Tano, Mia Moja Themanini na Moja Elfu (4,023,255,181,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Saba Arobaini na Tatu, Milioni Mia Nne Arobaini na Tano, Mia Tatu Hamsini na Mbili Elfu (743,445,352,000) ni za Miradi ya Maendeleo.

137.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Bunge la Jamhuri ya Muungano inaombewa jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Saba, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu (177,337,309,000) kwa ajili ya Mfuko  wa  Bunge  ambapo  Shilingi Bilioni Mia Moja na Sitini na Tisa, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu (169,337,309,000) ni za Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Nane (8,000,0000,0000) ni za Miradi ya Maendeleo.

MUHTASARI
138.       Mheshimiwa Spika, kwa muhtasari, naomba sasa Bunge lako Tukufu likubali kuidhinisha Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2015/2016 ya jumla ya Shilingi Trilioni Tano, Bilioni Mia Saba Sitini na Tatu, Milioni Mia Saba Themanini na Nne, na Sabini Elfu (5,763,784,070,000) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa; na jumla ya Shilingi Bilioni Mia Moja Sabini na Saba, Milioni Mia Tatu Thelathini na Saba, Mia Tatu na Tisa Elfu (177,337,309,000)  kwa ajili ya Mfuko wa Bunge, ikiwa ni Matumizi ya Kawaida na Fedha za Maendeleo za Ndani na Nje kwa ujumla wake.

139.      Mheshimiwa Spika, pamoja na Hotuba hii, yapo Majedwali ambayo yanafafanua kwa kina Makadirio ya Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake, Ofisi ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Bunge.

Mhe