Tuesday, December 01, 2015

WAZIRI MKUU MSTAAFU AKABIDHI OFISI KWA MAJALIWA



WAZIRI MKUU mstaafu Mizengo Pinda amekabidhi ofisi kwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa na kumtaka aimarishe ufuatiliaji wa maelekezo anayoyatoa kwenda ngazi za chini.

Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jana jioni (Jumatatu, Novemba 30, 2015), kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Bw. Pinda alisema katika kipindi cha uongozi wake kulikuwa na ucheleweshaji wa kupata majibu kutoka ngazi ya chini katika maelekezo aliyokuwa akitoa.

“Ofisi ya Waziri Mkuu ni kubwa na ina mambo mengi ya kufuatilia. Kama kuna changamoto nilikumbana nayo ni ucheleweshaji wa majibu kutokana na maagizo niliyokuwa nikitoa. Itabidi uwe makini sana katika kufuatilia hili,” alisema Waziri Mkuu mstaafu.

Alimtaka ahakikishe kila idara inakuwa na mpango kazi na kunakuwa na ufuatiliaji wa kila kilichopangwa. “Pia ninashauri uandaliwe kikao na watu wa Hazina ili wakueleze jinsi bajeti ya Serikali inavyoandaliwa ili iwe rahisi kwako kufuatilia vipengele kadhaa vya bajeti ya Serikali pindi maswali yanapoulizwa bungeni,” alisema.

Pia alimkabidhi taarifa yenye kurasa 104 ambayo inaelezea majukumu mbalimbali ya taasisi na idara zilizo chini ya Ofisi wa Waziri Mkuu. Ofisi ya Waziri Mkuu ina taasisi nane, idara nane na vitengo saba. Taasisi hizo ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Tume ya Kuratibu na Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS), Tume ya Uchaguzi (NEC) na Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA). Nyingine ni Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Baraza la Biashara la Taifa (TNBC) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Idara zilizopo kwenye ofisi hiyo ni Utawala na Rasimali watu, Sera na Mipango, Uratibu wa Maadhimisho ya Kitaifa na Sekta binafsi na Uwezeshaji. Nyingine ni Bunge na Siasa, uatibu wa shughuli za Serikali, Mpigachapa Mkuu wa Serikali na Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu.

Alisema pia ameridhishwa na kasi ya utendaji kazi ambayo Rais Dk. John Pombe Magufuli na Waziri Mkuu wameanza nayo na kwamba ana imani kwa uchapakazi wao na uadilifu wao,  anaamini wataweza kuivusha Tanzania na kuifikisha kwenye uchumi wa kati ambako Serikali imejielekeza kufika.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimshukuru Waziri Mkuu mstaafu na kumuahidi kutekeleza yote yaliyomo kwenye taarifa aliyomkabidhi. Pia aliahidi kusimamia kwa karibu suala la ufuatiliaji wa maelekezo anayotoa pamoja na yale yanayotoka ngazi za juu.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu, Dk. Florens Turuka, Naibu Katibu Mkuu (OWM), Bibi Regina Kikuli, wakuu wa taasisi zote nane, wakuu wa idara na vitengo vya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Wasaidizi wa Waziri Mkuu walioko ofisi yake binafsi.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,

FEDHA ZA SIKU YA UHURU KUJENGA BARABARA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameamuru fedha zilizopaswa kutumika kugharamia shamra shamra za siku ya Uhuru ambazo zingefanyika tarehe 09 Desemba 2015, kutumika kufanya upanuzi wa barabara ya Mwenge hadi Morocco jijini Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 4.3 kwa kuongeza njia mbili za barabara za lami.
Tayari fedha hizo kiasi cha shilingi bilioni nne zimepelekwa kwa wakala wa barabara hapa nchini TANROADS kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, linalopaswa kuanza mara moja
Akizungumza na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi PATRICK MFUGALE Ikulu Jijini Dar es Salaam, Dkt. Magufuli ametaka ujenzi wa barabara hiyo uanze haraka ili kukabiliana na adha ya msongamano wa magari katika  barabara hiyo
Kujengwa kwa njia hizo kutaifanya barabara ya Morroco hadi Mwenge kuwa na njia tano.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mstaafu wa Chama Cha wananchi (CUF) Prof. Ibrahim Lipumba Ikulu Jijini Dar es salaam.
Katika Mazungumzo hayo Prof. Lipumba amempongeza Dkt. Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na pia kwa kutoa hotuba nzuri ya uzinduzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyokonga nyoyo za Watanzania.
Kwa Upande wake Rais Magufuli amempongeza Prof. Lipumba kwa msimamo wake thabiti wa kupinga ufisadi na amemtakia heri katika shughuli zake.